• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:47 PM
Mswada walenga kuzima waajiri kuhamisha wafanyakazi ghafla

Mswada walenga kuzima waajiri kuhamisha wafanyakazi ghafla

NA CHARLES WASONGA

WAAJIRI watahitajika kuwapa wafanyakazi wao notisi ya miezi sita kabla ya kuwahamisha kutoka kituo kimoja hadi kingine ikiwa mswada uliopendekezwa utapitishwa na wabunge na utiwe saini na Rais kuwa sheria.

Mswada huo ambao umedhaminiwa na Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa unapania kuzima mienendo ya baadhi ya waajiri kuwahamisha wafanyakazi kama njia ya kuwaadhibu.

“Mswada wangu unalenga kuifanyia marekebisho Sheria ya Uajiri ili kumlazimu mwajiri ampe mfanyakazi notisi ya miezi sita kabla ya kumhamisha kutoka sehemu moja hadi nyingine. Mfanyakazi atatumia muda huu kufanya matayarisho kama kama vile kuwatafutia watoto wake shule katika sehemu akayohamishiwa,” Bw Barasa akaambia Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Leba mnamo Jumanne, Agosti 1, 2023 katika Majengo ya Bunge, Nairobi.

Mbunge huyo alikuwa amefika mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Runyenjes Eric Muchangi kutoa ufafanuzi kuhusu mswada huo.

Aliyevalia kilemba cheupe ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Kuhusu Leba Eric Muchangi akiongoza kikao cha kumsikiliza Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa akitetea mswada wake. PICHA | MAKTABA

Bw Barasa aliiambia kamati hiyo kuwa endapo uhamisho wa wafanyakazi unalenga kuimarisha kiwango cha utoaji huduma, basi mfanyakazi anafaa kupewa muda wa kujitayarisha.

“Huu mtindo wa baadhi ya waajiri wa kutumia uhamisho wa wafanyakazi kama njia ya kuwaadhibu wafanyakazi wao unakiuka haki za kibinadamu na utu. Ikiwa mfanyakazi amedhihirisha utepetevu au ametenda kosa fulani, anafaa kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa bali sio kuhamishwa kwingineko ghafla,” akaeleza.

Hata hivyo, Bw Barasa sheria hiyo haitatumika ikiwa katika hali ambapo mfanyakazi ndiye ameomba ahamishwe kutoka kituo kimoja hadi kingine kutokana na sababu za kiafya.

“Aidha, sheria hii haitatumika katika hali ambapo uhamisho wa mfanyakazi fulani unafanywa kutokana na sababu za kiusalama; watu fulani wanapotishia maisha yake,” akaongeza.

Hata hivyo, Bw Muchangi (mwenyekiti) alisema miezi sita ambayo Bw Barasa amependekeza katika mswada wake ni mrefu zaidi, haswa kwa wafanyakazi wanaofanyakazi katika sekta ya usalama.

“Kwa mtazamo wangu pendekezo la Bw Barasa halitafaa sekta ya usalama kama vile Idara ya Polisi na Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF). Maafisa katika sekta hizo ni watu ambao wanaweza kuhamishiwa sehemu yoyote kwa dharura kutokana na sababu za kiusalama,” akasema.

Hata hivyo, wabunge Lilian Siyoi (Mbunge Mwakilishi wa Trans Nzoia), Peter Kihungi (Kangema), Fabia Mule (Kangundo) waliunga mkono mswada huo wakisema utaokoa familia nyingi ambavyo zimevurugwa na “uhamisisho katili”.

Hata hivyo, wabunge James K’oyoo (Muhoroni) na Leah Sankale (Mbunge Mwakilishi wa Kajiado) walisema kwa Bw Barasa alipuuza kile walichodai kama haki ya waajiri kuimarisha utendekeza kupitia uhamisho wa wafanyakazi wao.

  • Tags

You can share this post!

Kenya Police Bullets FC kutaja kikosi cha msimu mpya Ijumaa

Refa Mary Njoroge kusimamia mchuano wa Argentina dhidi ya...

T L