• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Rupia aibuka mchezaji bora wa Desemba ligini

Rupia aibuka mchezaji bora wa Desemba ligini

Na GEOFFREY ANENE

MSHAMBULIAJI wa AFC Leopards Elvis Baranga Rupia ndiye mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa mwezi wa Desemba.

Machapo, jinsi Rupia anafahamika kwa jina la utani, alitinga mabao matano Desemba 2020 pamoja na moja katika siku ya kufungua msimu 2020-2021 mnamo Novemba 28 dhidi ya Tusker.

Alianza Desemba kwa kutikisa nyavu za wageni Bidco United mara mbili katika ushindi wa Ingwe wa 2-0 Desemba 6.

Alifuatiliza ukatili wake kwa kupachika mabao matatu katika mechi iliyofuata ambayo Ingwe ilirarua “Batoto ba Mungu” Sofapaka 3-0 Desemba 12.

Mchezaji huyu wa zamani wa Muhoroni Youth, Nakuru All Stars, Nzoia Sugar na Wazito, na Power Dynamos nchini Zambia, alitangaza wiki chache zilizopita kuwa atafukuzia kuibuka mfungaji bora kwenye Ligi Kuu ya msimu 2020-2021. Amefungia Ingwe mabao 10 kati ya 13 mabingwa hao wa zamani wa Kenya wamepata ligini msimu huu katika mechi tisa.

Rupia amepata mabao mengine dhidi ya Tusker (penalti), KCB (mawili), Kariobangi Sharks (moja) na Posta Rangers (moja).

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25 yuko mabao mawili nyuma ya Eric Kapaito wa Kariobangi Sharks katika vita vya kuwania taji la mfungaji bora msimu huu kwenye ligi hiyo ya klabu 18.

Alibwaga Joseph Okoth (KCB) na Kapaito katika tuzo ya Desemba na kutunukiwa Sh50,000.

Hajawahi kuchezea timu ya taifa ya Kenya almaarufu Harambee Stars. Alikuwa kwenye benchi Stars ikiduwaza Chipolopolo ya Zambia 2-1 katika mechi ya kirafiki jijini Nairobi mnamo Oktoba 9, 2020.

Kocha Jacob ‘Ghost’ Mulee amemjumuisha katika kikosi kinachojiandaa kwa mechi mbili za mwisho za kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) 2022 dhidi ya Misri na Togo.

Kenya itaalika Misri mnamo Machi 22 kabla ya kuelekea Lome mnamo Machi 30. Stars inahitaji zaidi ya muujiza kuingia AFCON kwa sababu imezoa alama tatu, tano nyuma ya Misri na Comoros zinazoshikilia nafasi mbili za kwanza. Timu mbili za kwanza kundi hilo la ‘G’ zitajikatia tiketi ya kuwa Cameroon kwa dimba hilo.

You can share this post!

Bayern Munich wakomoa Tigres UANL na kutwaa Kombe la Dunia

Tutakuwa tumedhibiti kero ya nzige kufikia Juni 2021...