• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Ryan Giggs ajiuzulu kama kocha wa timu ya taifa ya Wales

Ryan Giggs ajiuzulu kama kocha wa timu ya taifa ya Wales

Na MASHIRIKA

RYAN Giggs amejiuzulu rasmi kama kocha wa timu ya taifa ya Wales.

Fowadi huyo wa zamani wa Manchester United mwenye umri wa miaka 48 aliacha kudhibiti mikoba ya Wales kwa muda mnamo Novemba 2020 baada ya kutiwa mbaroni kwa tuhuma za kumdhulumu kimapenzi aliyekuwa mchumba wake, Kate Greville, kati ya Agosti 2017 na Novemba 2020.

Baada ya tukio hilo, Robert Page alipokezwa majukumu ya kudhibiti mikoba ya Wales kwa muda na akaongoza kikosi hicho kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu 1958.

“Shirikisho la Soka la Wales (FAW) linashukuru Giggs kwa kazi nzuri aliyotufanyia akidhibiti mikoba ya kikosi chetu. Kujiuzulu kwake kunaashiria kwamba yeye hana ubinfasi na anawazia sana mafanikio ya kikosi,” ikasema sehemu ya taarifa ya FAW.

Page, 47, alikuwa nahodha wa zamani wa Wales na akaaminiwa kuwa kocha msaidizi chini ya Giggs mnamo Agosti 2019. Alianza kusimamia mechi za Wales mnamo Novemba 2020 na akaongoza kikosi hicho kukamilisha kampeni za kundi lao kwenye Nations League kileleni.

Aliendelea kuwa msaidizi wa Giggs – aliyeteuliwa na Wales mnamo Januari 2018 – mnamo Machi 2021 Wales walipoanza kampeni zao za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar mnamo Novemba-Disemba 2022.

Kampeni hizo zilikamilika kwa ushindi dhidi ya Ukraine katika mchujo wa mwisho wa kufuzu mnamo Juni 2022. Itakuwa mara ya kwanza baada ya miaka 64 kwa Wales kunogesha Kombe la Dunia.

Wales wametiwa katika Kundi B kwenye Kombe la Dunia pamoja na Uingereza, Amerika na Iran. Watafungua rasmi kampeni zao dhidi ya Amerika mnamo Novemba 21, 2022.

Chini ya Page, Wales walitinga hatua ya 16-bora ya fainali za Euro 2020 zilizocheleweshwa hadi Juni-Julai 2021 kwa sababu ya janga la corona. Sasa anatazamiwa kuwa kocha wa Wales kwa mkataba wa kudumu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Marais wa EAC waunda kikosi cha kulinda amani DRC

TUSIJE TUKASAHAU: IEBC haijatoa ripoti kuhusu madai ya...

T L