• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Salah, Messi na Lewandowski kupigania tuzo ya Fifa ya Mchezaji Bora wa Mwaka 2021

Salah, Messi na Lewandowski kupigania tuzo ya Fifa ya Mchezaji Bora wa Mwaka 2021

Na MASHIRIKA

FOWADI wa Liverpool, Mohamed Salah na mshambuliaji matata wa timu ya wanawake ya Chelsea, Sam Kerr, ni miongoni mwa wanasoka ambao wamejumuishwa katika orodha ya wawaniaji wa tuzo zitakazotolewa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kwa Mwanasoka Bora wa Mwaka 2021.

Salah amejumuishwa katika orodha ya wawaniaji wa kiume pamoja na nyota Lionel Messi wa Paris Saint-Germain (PSG) na supastaa wa Bayern Munich, Robert Lewandowski.

Kerr ameteuliwa pamoja na wanasoka wawili mahiri wa Barcelona Jennifer Hermoso na Alexia Putellas katika kitengo cha wanawake.

Washindi watatangazwa wakati wa kutolewa kwa tuzo hizo za Best Fifa Football Awards jijini Zurich, Uswisi mnamo Januari 17, 2022.

Salah kwa sasa ndiye anaongoza orodha ya wafungaji bora wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu kwa mabao 16 baada ya kuambulia nafasi ya pili nyuma ya Harry Kane wa Tottenham Hotspur mnamo 2020-21.

Kwa upande wake, Kerr ambaye ni raia wa Australia, aliongoza Chelsea kuhifadhi ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake nchini Uingereza (WSL) mnamo 2021 na kutinga fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Washindi wa tuzo hizo hupigiwa kura na makocha wa timu za taifa, manahodha wa timu za taifa, wanahabari na mashabiki.

Lewandowski alishinda tuzo hiyo mnamo 2020 huku Lucy Bronze wa Manchester City na timu ya taifa ya Uingereza akitawazwa mshindi wa kitengo cha wanawake mwaka huo.

Erik Lamela wa Tottenham Hotspur amejumuishwa katika orodha ya wawaniaji wa tuzo ya FIFA Puskas ambayo hutolewa kwa bao zuri zaidi kila mwaka. Bao lake katika gozi la EPL dhidi ya Arsenal mnamo Machi 2021 linapigania tuzo hiyo.

ORODHA YA WAWANIAJI WA TUZO ZA FIFA:

Mchezaji Bora wa Kike:

  • Jennifer Hermoso (Uhispania/Barcelona)
  • Sam Kerr (Australia/Chelsea)
  • Alexia Putellas (Uhispania/Barcelona)

Mchezaji Bora wa Kiume:

  • Robert Lewandowski (Poland/Bayern Munich)
  • Lionel Messi (Argentina/Barcelona/Paris St-Germain)
  • Mohamed Salah (Misri/Liverpool)

Kocha Bora wa Kike:

  • Lluis Cortes (Uhispania/Barcelona)
  • Emma Hayes (Uingereza/Chelsea)
  • Sarina Wiegman (Uholanzi/Timu ya taifa ya Uholanzi/Timu ya taifa ya Uingereza)

Kocha Bora wa Kiume:

  • Pep Guardiola (Uhispania/Manchester City)
  • Roberto Mancini (Italia/Timu ya taifa ya Italia)
  • Thomas Tuchel (Ujerumani/Chelsea)

Kipa Bora wa Kike:

  • Ann-Katrin Berger (Ujerumani/Chelsea)
  • Christiane Endler (Chile/Paris Saint-Germain/Lyon)
  • Stephanie Labbe (Canada/FC Rosengard/Paris Saint-Germain)

Kipa Bora wa Kiume:

  • Gianluigi Donnarumma (Italia/AC Milan/Paris Saint-Germain)
  • Edouard Mendy (Senegal/Chelsea)
  • Manuel Neuer (Ujerumani/Bayern Munich)

Tuzo ya Fifa Puskas

  • Erik Lamela – Tottenham (dhidi ya Arsenal, Machi 14, 2021)
  • Patrik Schick – Czech Republic (dhidi ya Scotland, Juni 14, 2021)
  • Mehdi Taremi – Porto (dhidi ya Chelsea, Aprili 13, 2021)

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Ndimi za sumu huhepa adhabu

Mboma apiku Kipchoge, Kipyegon na kutawazwa Mchezaji Bora...

T L