• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:46 PM
Salah na De Bruyne kati ya masogora wanane wanaowania taji la Mchezaji Bora wa Mwaka katika EPL

Salah na De Bruyne kati ya masogora wanane wanaowania taji la Mchezaji Bora wa Mwaka katika EPL

Na MASHIRIKA

KEVIN de Bruyne wa Manchester City na Mohamed Salah wa Liverpool ni miongoni mwa masogora wanane ambao wameteuliwa kuwania taji la Mchezaji Bora wa Mwaka wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu.

De Bruyne na Salah wote wamewahi kushinda taji hilo. Man-City na Liverpool kila moja ina wachezaji wawili katika orodha hiyo inayojumuisha Joao Cancelo (Man-City) na Trent Alexander-Arnold (Liverpool).

Wengine ni fowadi wa West Ham United, Jarrod Bowen, mvamizi wa Arsenal, Bukayo Saka, mshambuliaji wa Tottenham Hotspur, Son Heung-min na nahodha wa Southampton, James Ward-Prowse.

Kufikia sasa, Man-City wanaselelea kileleni mwa jedwali la EPL kwa alama 89, tatu zaidi kuliko nambari mbili Liverpool. Zimesalia mechi mbili pekee kabla ya kampeni za EPL msimu huu kutamatika rasmi.

Salah ambaye ni raia wa Misri anaongoza orodha ya wafungaji bora wa EPL baada ya kupachika wavuni mabao 22 huku De Bruyne akiwa na magoli 15 pamoja na kuchangia saba mengine kufikia sasa muhula huu.

De Bruyne na Salah waliunga tena orodha ya tuzo hiyo mnamo 2020-21 ila wakalambishwa sakafu na beki mzoefu wa Man-City, Ruben Dias.

Mshindi wa tuzo hiyo huamuliwa na kura za umma zinazopigwa kupitia tovuti ya EPL pamoja na kura za jumla kutoka kwa manahodha 20 wa vikosi vya EPL na jopo la wataalamu wa soka.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Esther Gathogo asema alijihisi kama mfungwa ndani ya UDA

Uchunguzi duni huvuruga kesi zinazohusu polisi – Haji

T L