• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:55 AM
AFCON: Senegal kuvaana na Burkina Faso kwenye nusu-fainali baada ya kudengua Equatorial Guinea

AFCON: Senegal kuvaana na Burkina Faso kwenye nusu-fainali baada ya kudengua Equatorial Guinea

Na MASHIRIKA

SENEGAL walijikatia tiketi ya kuvaana na Burkina Faso kwenye nusu-fainali ya Kombe la Afrika (AFCON) baada ya kupokeza Equatorial Guinea kichapo cha 3-1 kwenye hatua ya nane-bora mnamo Jumapili usiku nchini Cameroon.

Fowadi wa zamani wa Bristol City, Famara Diedhiou aliwaweka Senegal kifua mbele katika dakika ya 28 baada ya kushirikiana na Sadio Mane.

Ingawa Equatorial Guinea walipokezwa penalti mwanzoni mwa kipindi cha kwanza, maamuzi hayo yalibatilishwa na teknolojia ya VAR. Hata hivyo, walisawazisha mambo kupitia Jannick Buyla katika dakika ya 57.

Beki Cheikhou Kouyate alitokea benchi na kuwarejesha Senegal uongozini katika dakika ya 68 kabla ya mvamizi Ismaila Sarr wa Watford kuzamisha kabisa chombo cha Equatorial Guinea katika dakika ya 79.

Senegal ambao hawajawahi kushinda taji la AFCON, sasa watavaana na Burkina Faso kwenye nusu-fainali ya kwanza mnamo Februari 2, siku moja kabla ya Misri kumenyana na Cameroon kwenye nusu-fainali nyingine. Fainali ya makala ya 33 ya AFCON mwaka huu itatandazwa Februari 6, 2022 uwanjani Olembe.

Equatorial Guinea wanaoshikilia nafasi ya 114 duniani, walishuka dimbani wakiwa na ari ya kuduwaza Senegal wanaoshikilia nafasi ya kwanza barani Afrika na 20 kimataifa. Walitinga nusu-fainali za AFCON mnamo 2015 wakiwa wenyeji.

Mane ambaye huchezea Liverpool katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), alikuwa akiwajibishwa kwa mara ya kwanza baada ya kupata jeraha la kichwa dhidi ya Cape Verde kwenye hatua ya 16-bora mnamo Januari 25, 2022.

Bao kutoka kwa Equatorial Guinea lilikuwa la kwanza kwa Senegal kufungwa kwenye kampeni za AFCON mwaka huu. Wanafainali hao wa 2002 na 2019 walifungua kampeni zao za Kundi B kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Zimbabwe kabla ya kuambulia sare tasa dhidi ya Guinea na Malawi. Walifuzu kwa robo-fainali baada ya kupepeta Cape Verde 2-0 katika hatua ya 16-bora.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Ruto ajigamba

Wandani wa Ruto sasa wanadai sheria ya vyama itawafaa,...

T L