• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Sharks, Homeboyz zalenga kupanua uongozi ligini leo

Sharks, Homeboyz zalenga kupanua uongozi ligini leo

Na CECIL ODONGO

VIONGOZI wa Ligi Kuu (KPL) Kariobangi Sharks na Kakamega Homeboyz leo watapata nafasi ya kuzidisha uongozi wao kwenye ligi, wakiwa wanakabiliana na wapinzani dhaifu.

Sharks walio juu kileleni kwa alama 16, wataikaribisha Kenya Police inayoshikilia nafasi ya 15, katika uga wa Kasarani mjini Nairobi kuanzia saa tisa jioni.Homeboyz, ambao bado hawajapoteza mchuano wowote na wana alama sawa na Sharks, nao watakuwa wenyeji wa Mathare United ugani Bukhungu, Kakamega.

Mabingwa wa zamani Sofapaka watachuana na Wazito kule Wundanyi huku Nairobi City Stars wakivaana na Nzoia Sugar ugani Ruaraka jijini Nairobi.Kiungo wa Sharks, Patilah Omotto, jana alisema wamekuwa na msururu ya matokeo mazuri hasa baada ya kushinda mechi tatu mfululizo dhidi ya Mathare United, Tusker na Nairobi City Stars.

“Polisi ni timu nzuri na siwezi kusema kuwa kwa sababu tumeshinda mechi tatu mfululizo, wao watakuwa mswaki kwetu. Katika mpira hauwezi kudharau timu yoyote ila sisi yetu ni kuweka bidii na kushinda,” Omotto akaeleza Taifa Leo.

Washambuliaji Felix Oluoch na Eric Mmata wamekuwa wakali wa Sharks, wakifunga maboa sita na nne mtawalia kwa vijana hao wa kocha William Muluya.Naye kocha wa Kenya Police John ‘Bobby’ Ogolla alisema kuwa timu yake imekuwa na matokeo duni ila analenga kuyabadili kuanzia mechi dhidi ya Sharks.“Sharks wanacheza kama Barcelona na hiyo inamaanisha kuwa lazima tuwe makini.

Tuliwanunua wachezaji wapya na bado hawajaingiliana vyema. Soka ni mchezo ambao hubadilika kila mara na nina imani tupata makali yetu na kuanza kupata matokeo mazuri,” akasema Ogolla.Kenya Police ambao walipandishwa ngazi msimu uliopita, wameshinda mechi moja pekee walipoilemea Nzoia Sugar 3-1 mnamo Oktoba.

Hii ni licha ya kuwanunua wachezaji wazoefu kama Clifton Miheso, beki Musa Mohamed, Kiungo Duke Abuya na mvamizi hatari John Mark Markwatta.Timu hiyo imekuwa na safu ya ulinzi inayovuja na wamechapwa mabao 11 huku wakifunga sita pekee.

Katika mechi zao saba wamekusanya alama nne pekee, tatu zaidi ya Vihiga Bullets inayoburura mkia.Mkufunzi wa Homeboyz Bernard Mwalala alisema kuwa wanatarajia mechi dhdi ya Mathare United inayoshikilia nafasi ya 13 itakuwa ngumu.

“Kucheza dhidi ya timu ambazo zinasuasua huwa ni ngumu kwa sababu lazima uwatayarishe wachezaji wako kisaikolojia. Mathare watakuja na moto wakitumai kuondoka eneo la hatari na kwa hivyo, tutaicheza mechi hiyo kwa umakinifu mkubwa,” akasema Mwalala.

RATIBA YA LEO:Nairobi City Stars v Nzoia Sugar (Ruaraka Grounds 1pm)Kariobangi Sharks v Kenya Police (MISC 3pm)Kakamega Homeboyz v Mathare United (Bukhungu Stadium 3pm)Sofapaka v Wazito (Wundanyi Stadium 3pm)

You can share this post!

Bellingham apigwa faini ya Sh5.3 milioni kwa kukosa maamuzi...

Team Control yabanwa Maluda Super Cup

T L