• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Simba SC yaelekea Afrika Kusini kurarua Kaizer Chiefs soka ya Klabu Bingwa Afrika

Simba SC yaelekea Afrika Kusini kurarua Kaizer Chiefs soka ya Klabu Bingwa Afrika

Na GEOFFREY ANENE

Mabingwa wa Tanzania, Simba SC wametua nchini Afrika Kusini mnamo Jumanne mchana tayari kuchuana na Kaizer Chiefs katika robo-fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mei 15, 2021.

Simba walitangaza kupitia Kenya wakielekea mjini Johannesburg. Klabu hiyo ambayo inatiwa makali na kocha Mfaransa Didier Gomes Da Rosa, imeajiri beki Joash Onyango na kiungo Francis Kahata. Wakenya hao wako katika kikosi cha wachezaji 24 kilichoondoka nchini Tanzania saa nne kasorobo asubuhi.

Chiefs, ambayo imeajiri kiungo Mkenya Anthony “Teddy” Akumu, itamenyana na Simba katika mechi ya mkondo wa kwanza ugani FNB mjini Johannesburg mnamo Mei 15.

Timu hizo zitarudiana uwanjani Benjamin Mkapa mjini Dar es Salaam mnamo Mei 22. Simba na Chiefs hawajawahi kukutana katika mashindano yoyote kwa hivyo itakuwa mara yao ya kwanza kabisa.

Vijana wa Gomes walijikatia tiketi ya robo-fainali baada ya kukamilisha mechi za Kundi A katika nafasi ya kwanza. Walifuzu kutoka kundi hilo pamoja na mabingwa watetezi Al Ahly kutoka Misri waliomaliza wa pili nao AS Vita (DR Congo) na Al Merreikh (Sudan) wakabanduliwa. Chiefs waliingia robo-fainali baada ya kukamilisha Kundi C katika nafasi ya pili nyuma ya Wamoroko Wydad. Wanashiriki robo-fainali kwa mara yao ya kwanza kabisa.

Robo-fainali nyingine zitakutanisha MC Alger (Algeria) na Wydad, CR Belouizdad (Algeria) dhidi ya Esperance (Tunisia) nayo Al Ahly itakabana koo na Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini). Sundowns imeajiri beki Mkenya Brian “Mandela” Onyango.

Kikosi cha Simba SC: Makipa – Aishi Manula, Beno Kakolanya na Ally Salim; Mabeki – Shomari Kapombe, Joash Onyango, Pascal Wawa, Ibrahim Ame, Erasto Nyoni, Gadiel Michael, Mohamed Hussein, Kennedy Juma na David Kameta; Viungo – Jonas Mkude, Rally Bwalya, Mzamiru Yassin, Luis Miquissone, Hassan Dilunga, Clatous Chama, Francis Kahata na Taddeo Lwanga; Washambuliaji – Meddie Kagere, John Bocco, Ibrahim Ajib na Chris Mugalu.

  • Tags

You can share this post!

Kiambu Community FC yakuza vipaji vya soka na kuhimiza...

Ratiba ya Kenya Simbas ya Kombe la Afrika 2021 ya kuingia...