• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 3:46 PM
Baadhi ya watumiaji mitandao ya kijamii wakerwa na agizo la Rais

Baadhi ya watumiaji mitandao ya kijamii wakerwa na agizo la Rais

Na MARY WANGARI

KENYA ilipoteza Sh560 bilioni kutokana na athari za janga la Covid-19, Rais Uhuru Kenyatta alisema mnamo Ijumaa, Machi 12, 2021.

Akihutubia taifa katika Ikulu Nairobi, mwaka mmoja tangu kisa cha kwanza cha maambukizi ya virusi vya corona kuripotiwa nchini, Rais Kenyatta alielezea matumaini kuhusu sekta ya uchumi nchini.

Alisema kuwa, licha ya madhara ya Covid-19, kuna matumaini ya sekta ya uchumi nchini kuimarika kwa asilimia saba mwaka huu wa 2021.

Rais alipiga marufuku mikusanyiko yote ya umma ikiwemo mikutano ya kisiasa, sherehe za harusi, mazishi na katika sehemu za ibada kwa kipindi cha siku 30.

Aidha, alitangaza kafyu kote nchini kuanzia saa tatu usiku kwa muda wa siku 60 zijazo, huku maeneo ya burudani yakifungwa kufikia saa tatu usiku.

Tangazo hilo kuhusu kuendelezwa kwa kafyu kote nchini lilionekana kuwakera Wakenya ambao wengi wao walikuwa wanasubiri kurejelea maisha ya kawaida kabla ya kuzuka kwa janga la corona.

Baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii walishangaa ni kwa nini Rais alisitisha mikutano ya kisiasa kwa mwezi mmoja ilhali kafyu aliipa miezi miwili.

“Unapiga marufuku mikutano ya kisiasa kwa siku 30 na kuongeza muda wa kafyu kwa siku 60. Sikujua corona hutembea usiku,” aliudhika Daniel Karuga.

“Alishauriwa vibaya. Kwani hii kafyu inasaidia na nini?” aliuliza Apollo Ole Rarrii.

Hata hivyo, baadhi walishangaa ni lini mikutano ya kisiasa ilipofunguliwa rasmi baada ya kupigwa marufuku mwaka 2020 kama mojawapo ya mikakati ya kuzuia Covid-19 kusambaa.

“Katika hotuba yake ya kwanza, alikuwa amesitisha mikutano yote ya kisiasa. Aliifungua tena lini? Sasa kwa sababu ameifunga tena, ataifungua rasmi au?” Charles Kagema alishangaa.

Yupo aliyehisi kuwa masharti hayo yanaleta kero.

“Sisi ni wafungwa katika taifa letu wenyewe. Inahuzunisha,” alilalamika Kenahy.

  • Tags

You can share this post!

Waandishi wa Thika wapewa hamasisho kuhusu wajibu wao

Sina uhakika iwapo Sergio Ramos atasalia kambini mwa Real...