• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:47 PM
Soko ya Daraja la Pili yapamba moto Pwani

Soko ya Daraja la Pili yapamba moto Pwani

NA CHARLES ONGADI

MOMBASA 

LIGI ya Taifa Daraja la Pili Kaskazini kundi A inaendelea kupamba moto katika viwanja mbalimbali Pwani huku timu zilizopigiwa upatu kupata ushindi zikirambishwa sakafu.

Shanzu United FC ambayo wiki iliyopita iliititiga Kilifi All Stars mabao 4-1, ilijipata ikisalimu amri mbele ya wenyeji wao Mariakani FC kwa bao 1-0 katika mchuano uliogaragazwa uwanjani Mariakani Village Polytechnic.

Hata hivyo, kocha mkuu wa Shanzu United James Ochieng’ Sewe ameiambia Taifa Leo Digitali kwamba kilichosababisha wao kutota ugenini ni kutokana na wao kufika uwanjani wakiwa wamechelewa.

“ Gari letu lilipata panchari barabarani hivyo kutulazimisha kuchelewa na kufika dakika chache mechi kuanza lakini wachezaji wangu wakajitahidi kadri ya uwezo wao kabla ya kusalimu amri,” akasema kocha Ochieng’.

Green Marine FC ambayo wiki iliyopita iliikung’uta Beach Bay ya Magarini, Malindi ilipigwa breki kwa kulishwa goli 1-0 na Kishada FC uwanjani Utange Primary, Kisauni siku ya jumapili.

Hata hivyo, Progressive FC ya Malindi illizidi kuonesha makeke yake katika ligi hii kwa kuicharaza Super Matuga mabao 4-0 kwao nyumbani Matuga.

Katika pambano lao la awali, Progressive iliinyuka Samburu Lions goli 1-0 ugani Alaskan, mjini Malindi huku ikikumbukwa kuilambisha Shanzu United 1-0 katika mechi yao ya ufunguzi.

Tikki Fc ya Taita Taveta iliipokeza Ziwani Youth ya Mombasa kibano cha mabao 2-0 katika mchuano uligaragazwa ugani Soweto Primary, Taita Taveta.

Kilifi All Stars inaendelea kurekebisha makosa madogo madogo baada ya kuanza michuano yake kwa mguu mbaya.

Kilifi all Stars iliitandiksa nacet FC kwa mabao 2-1 katika mechi ya kusisimua iliyochezwa uwanjani MTG, Mnarani, Kilifi.

Masaibu ya Bahari FC katika ligi hii yalizidi kuendelea pale waliponyukwa na wenyeji wao Maji Bombers kwa mabao 2-1.

Wiki iliyopita Bahari FC ilijipata ikitota mbele ya mashabiki wake wa nyumbani kwa kulishwa magoli 3-1 na Mariakani FC uwanjani Mtwapa Primary.

Matokeo mengine ni kwamba Yanga FC ya Malindi na Samburu Lions ziliumiza nyasi bure baada ya kutoka sare 0-0 uwanjani Alaskan, Malindi nayo Borrussia Dortmund ya Shariani ikaandikisha matokeo sawia na hayo huu Shariani, Kilifi.

Wakati huo huo, kinyang’anyiro cha kuwania kiatu cha dhahabu katika ligi hii inazidi kupamba moto huku wachezaji sita wakiwa na mabao tatu kila mmoja.

Collins Hajuu Anthony wa Mariakani FC, Heri Juma (Shanzu United), Omar Mwarere (Kilifi All Stars),Mwatunza Ali (Super Matuga), Hassan Mwambengu (Maji Bombers) na Eddyson Katana wa Progressive kufika sasa wamecheka na nyavu mara tatu kila mmoja.

Michuano hii inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Nchini (FKF) itaendelea kurindimwa wiki hii katika viwanja mbali mbali jimbo la Pwani.

You can share this post!

Mchecheto mitandaoni Karen Nyamu akijaribu kumnasa Samidoh

MMvita Youngstars yailima Annex 07 FC 3-0