• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 11:34 AM
St Johnstone kuonana na Hibernian kwenye fainali ya Scotiish Cup

St Johnstone kuonana na Hibernian kwenye fainali ya Scotiish Cup

Na MASHIRIKA

MABAO mawili chini ya dakika mbili za kipindi cha pili yalisaidia St Johnstone kuchabanga St Mirren 2-1 na kufuzu kwa fainali ya Scottish Cup mnamo Jumapili huku wakiweka hai matumaini ya kutwaa jumla ya mataji mawili muhula huu.

Chris Kane aliwafungulia St Johnstone walionyakua taji la League Cup mnamo Februari 28, 2021 ukurasa wa mabao katika dakika ya 72 kabla ya Glenn Middleton kufunga la pili dakika mbili baadaye.

Ingawa Conor McCarthy alifungia St Mirren katika dakika ya 86, juhudi zake hazikuzuia St Johnstone kujikatia tiketi ya fainali ambayo kwa sasa itawakutanisha na Hibernian mnamo Mei 22.

 St Mirren hawajawahi kushinda mechi yoyote ya nusu-fainali za Scottish Cup tangu 1987 walipotawazwa wafalme wa kipute hicho.

Hibernian walitinga fainali ya Scottish Cup kwa mara ya kwanza tangu 2016 baada ya kuwapokeza Dundee United kichapo cha 2-0 kwenye nusu-fainali.

Chini ya kocha Jack Ross, Hibernian walifunga mabao yao kupitia kwa Kevin Nisbet na Christian Doidge katika dakika za 27 na 58 mtawalia.

Lawrence Shankland alipoteza nafasi nyingi za kurejesha Dundee United mchezoni huku fataki zake zikidhibitiwa vilivyo na kipa Matt Macey wa Hibernian.

Baada ya kulazimika kusubiri kwa miaka 114 kabla ya kutia kapuni taji lao la kwanza mnamo 2016, Hibernian kwa sasa wana fursa nzuri ya kutawazwa mabingwa wa Scottish Cuo kwa mara ya pili chini ya kipindi cha miaka mitano.

Zikisalia mechi mbili pekee kwa kampeni za Ligi Kuu ya Scotland msimu huu kukamilika rasmi, Dundee United wamepangiwa kuwa wenyeji wa Motherwell mnamo Mei 12 huku Hibernian wakivaana na Aberdeen ugenini. Kwa upande wao, St Mirren watakuwa wageni wa Kilmarnock huku St Johnstone wakiwaendea Celtic.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Everton wakomoa West Ham ligini na kuweka hai matumaini ya...

Man-United wapiga Aston Villa na kujipa uhakika wa...