• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 6:55 AM
Man-United wapiga Aston Villa na kujipa uhakika wa kushiriki kipute cha UEFA

Man-United wapiga Aston Villa na kujipa uhakika wa kushiriki kipute cha UEFA

Na MASHIRIKA

MANCHESTER United walijipa uhakika wa kukamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ndani ya orodha ya nne-bora msimu huu kwa kutoka nyuma na kuwapokeza Aston Villa kichapo cha 3-1 mnamo Jumapili ugani Villa Park.

Ushindi huo wa Man-United pia unawaweka Manchester City katika ulazima wa kusubiri zaidi kabla ya kutawazwa mabingwa wa EPL msimu huu wa 2020-21.

Mabao ya Man-United ambao tayari wamefuzu kwa fainali ya Europa League itakayowakutanisha na Villarreal ya Uhispania yalifumwa wavuni na Bruno Fernandes, Mason Greenwood na Edinson Cavani aliyetokea benchi katika kipindi cha pili.

Alama tatu zilizovunwa na Man-United dhidi ya Villa na kichapo cha 1-0 ambacho Everton walipokeza West Ham United ziliwapa masogora wa kocha Ole Gunnar Solskjaer uhakika wa kunogesha soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) muhula ujao wa 2021-22.

Iwapo Man-United wangepoteza dhidi ya Villa, basi Man-City waliopigwa na Chelsea 2-1 mnamo Mei 8, 2021 ugani Etihad wangalijizolea ubingwa wa EPL. Hata hivyo, bao la Bertrand Traore katika dakika ya 24 halikutosha kusaidia Villa kuzamisha chombo cha Man-United ambao kwa sasa wana alama 70, saba zaidi kuliko nambari nne Leicester City.

Ni pengo la alama 10 ndilo linatamalaki kati ya Man-United na viongozi wa jedwali Man-City. Mwanya huo huenda ukafikia pointi nne pekee iwapo Man-United watakomoa Leicester na Liverpool katika mechi mbili zijazo kabla ya Man-City ya kocha Pep Guardiola kurejea ugani kupepetana na Newcastle United ugani St James’ Park.

Aston Villa kwa upande wamepangiwa kualika Everton mnamo Mei 13 kabla ya kuwaendea Crystal Palace ugani Selhurst Park siku tatu baadaye.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

St Johnstone kuonana na Hibernian kwenye fainali ya...

Ajax na Man-United katika vita vya kumsajili fowadi mahiri...