• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
STAA WA SPOTI: Malkia wa kipekee katika marathon

STAA WA SPOTI: Malkia wa kipekee katika marathon

NA GEOFFREY ANENE

NYOTA Ruth Chepng’etich ni mmoja wa wanariadha ambao Kenya imechagua kupeperusha bendera ya taifa kwenye Riadha za Dunia nchini Amerika mwezi Julai.

Malkia huyo wa mbio ndefu kutoka Idara ya Magereza atakuwa akitetea taji alilonyakua Qatar 2019.

Chepng’etich anayefanyia mazoezi katika milima ya Ngong viungani mwa jiji la Nairobi, ni bingwa wa Chicago Marathon na mshindi wa nishani ya shaba kwenye Riadha za Nusu-Marathon Duniani 2018 na alitwaa medali ya shaba katika mbio za London Marathon 2020.

Amevuna mataji mengi katika mbio za masafa marefu zikiwemo Standard Chartered Dubai Marathon 2019 na Nagoya Marathon mnamo Machi 2022 alipokosa rekodi ya dunia ya kinadada pekee pembamba baada ya kukamilisha kwa saa 2:17:08 na 2:17:18 mtawalia.

Rekodi ya dunia ya marathon ya kinadada pekee ya 2:17:01 inashikiliwa na Mkenya Mary Keitany tangu Aprili 2017.

Chepng’etich, ambaye alivuna Sh28 milioni mjini Nagoya, Japan, amekuwa kwenye riadha miaka minane.

Alizamia mchezo huu kikamilifu baada ya shule ya upili.

“Nilipenda karibu kila mchezo – netiboli, mbio, soka…Hata hivyo, niliamua kuchukulia riadha kwa uzito nilipokamilisha kidato cha nne mwaka 2014,” anasema.

Mtimkaji huyo alianza kuona matunda 2018 alipoibuka nambari mbili katika mbio za kilomita 10 za makumbusho ya bingwa wa marathon ya Olimpiki ya 2008 Samuel Wanjiru mwaka 2018.

Kisha, Chepng’etich alipata ushindi wake wa kwanza katika mashindano makubwa aliposhiriki Istanbul Marathon 2017.

Tangu wakati huo, Chepng’etich amekuwa akifanya vyema.

Kwa miezi sita, Chepng’etich alishikilia rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 21 baada ya kushinda Istanbul Half Marathon kwa saa 1:04:02 April 4, 2021.

Itakumbukwa Chepng’etich hakumaliza marathon kwenye Olimpiki mnamo Agosti 7, 2021.

“Huo ndio ulikuwa wakati wangu mbaya katika riadha. Sikukamilisha mbio kwa sababu ya jeraha na pia nilipata ugonjwa wa Covid-19,” alieleza.

  • Tags

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Raila anajiharibia kwa kuhujumu wagombeaji...

GUMZO: Dalili zaongezeka Pogba ataondoka United

T L