• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Sundowns anayochezea Mkenya Brian Mandela yapiga maadui Orlando Pirates

Sundowns anayochezea Mkenya Brian Mandela yapiga maadui Orlando Pirates

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA watetezi Mamelodi Sundowns walijinyanyua kutoka kichapo dhidi ya Kaizer Chiefs kwa kulipua mahasimu wa tangu jadi Orlando Pirates 3-0 kwenye Ligi Kuu ya Afrika Kusini, Jumapili.

Sundowns, ambao walimpa beki Mkenya Brian ‘Mandela’ Onyango dakika nane za mwisho, walivuna ushindi kupitia mabao ya Ricardo Nascimento, Peter Shalulile na Lyle Lakay ugani Orlando, Johannesburg.

“The Brazilians” jinsi timu hiyo inafahamika kwa jina la utani, ilipata bao la kwanza kupitia penalti ya Mbrazil Nascimento baada ya beki wa Pirates Innocent Maela kunawa shuti la Shalulile ndani ya kisanduku chake dakika ya 57.

Shalulile aliimarisha uongozi wa Sundowns dakika ya 76 baada ya beki Thulani Hlatshwayo kupokonywa mpira na Gift Motupa ambaye alimegea Mnamibia huyo pasi safi aliyoikamilisha kwa ustadi.

Lakay alihitimisha maangamizi hayo dakika ya 80, huku Mandela akiingizwa uwanjani kujaza nafasi ya Nascimento dakika ya 82.

Ushindi huo ni wa tatu mfululizo wa Sundowns dhidi ya Pirates msimu huu baada ya kuwalima 1-0 katika mechi ya mkondo wa kwanza Januari 2 na kuwapepeta 4-1 kwenye Kombe la Nedbank mnamo Aprili 15.

Sundowns ya kocha Manqoba Mngqithi inaongoza ligi hiyo ya klabu 16 kwa alama 51 baada ya kujibwaga uwanjani mara 24.

Inafuatiwa na AmaZulu (pointi 50) na Golden Arrows (43) ambazo zimesakata michuano 26 kila moja, Moroka Swallows (40) kutokana na mechi 25 nayo Pirates inakamilisha mduara wa tano-bora kwa kujizolea alama 39 baada ya kucheza mechi 24.

Kaizer Chiefs anayochezea kiungo Mkenya Anthony ‘Teddy’ Akumu inakamata nafasi ya tisa kwa alama 29 kutokana na mechi 25.

You can share this post!

Difaa anayochezea Mkenya Masud Juma yamaliza ukame wa mechi...

Wanasoka waomba kazi kwenye mradi wa ukarabati wa uwanja wa...