• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Theo Walcott apokezwa mkataba wa kudumu ugani St Marys kwa matarajio ya kuwa kocha wa baadaye wa Southampton

Theo Walcott apokezwa mkataba wa kudumu ugani St Marys kwa matarajio ya kuwa kocha wa baadaye wa Southampton

Na MASHIRIKA

FOWADI Theo Walcott amesajiliwa upya na Southampton kwa mkataba wa kudumu na matazamio ni kwamba ataishia kuwa kocha kambini mwa kikosi hicho ambacho kwa sasa kinatiwa makali na mkufunzi Ralph Hasenhuttl.

Walcott, 32, amewajibikia Southampton almaarufu ‘The Saints’ msimu huu kwa mkopo kutoka Everton ambao chini ya kocha Sam Allardyce, walimsajili kutoka Arsenal kwa Sh2.8 bilioni mnamo 2018.

Carlo Ancelotti ambaye ni kocha wa sasa wa Everton hakuwa na mipango yoyote ya baadaye kumhusu Walcott uwanjani Goodison Park.

Walcott ambaye ni raia wa Uingereza, sasa anarejea ugani St Mary’s alikoanzia taaluma yake ya usogora kabla ya Arsenal kujitwalia huduma zake kwa kima cha Sh1.7 bilioni pekee mnamo 2006.

Kwa mujibu wa taarifa ya Southampton, Walcott atakuwa sasa anaandaliwa kuwa kocha wa baadaye wa Southampton chini ya Hasenhuttl atakayekuwa pia akimwajibisha mara kwa mara katika baadhi ya mechi za msimu ujao wa 2021-22.

Walcott aliweka historia ya kuwa mchezaji mchanga zaidi kuwahi kuchezea kikosi cha kwanza cha Southampton akiwa na umri wa miaka 16 na siku 143 pekee alipotokea benchi dhidi ya Wolves katika mchuano wa Ligi ya Daraja la Kwanza (Championship) uliokamilika kwa sare tasa mnamo 2005.

Akiwa Arsenal, alisaidia kikosi hicho kutwaa mataji mawili ya Kombe la FA na akawajibishwa mara 47 na timu ya taifa ya Uingereza.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Masogora tisa wanaopiga soka ya EPL waitwa kambini mwa timu...

Raila asuta polisi kwa ukatili wao katika chaguzi ndogo