• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Timu tatu za voliboli kukosa mastaa kwenye kipute muhimu

Timu tatu za voliboli kukosa mastaa kwenye kipute muhimu

Na JOHN KIMWERE

TIMU tatu za voliboli ya wanawake za humu nchini zitakosa huduma za baadhi ya wachezaji muhimu kwenye ngarambe ya Klabu Bingwa Afrika (CAVB) baadaye mwezi huu. Kipute hicho kimeratibiwa kuandaliwa mwezi Aprili 19 -Mei 1 mwaka huu jijini Sousse, Tunisia.

Klabu za Kenya Prisons, Kenya Pipeline na KCB zitakosa huduma za wachezaji wazo walio katika kikosi cha taifa cha Malkia Strikers kinaojiandaa kushiriki mashindano ya Olimpiki mjini Tokyo, Japan mwezi Julai mwaka huu. Meneja wa Malkia Strikers, Alfred Chedotum anasema kuwa vipusa walio kambini hawataruhusiwa kujiunga na klabu zao kutokana na masharti ya kuzuia msambao wa virusi hatari vya corona.

NAHODHA WA MALKIA WA STRIKERS

”Kufuatia tishio la virusi vya corona vinavyochangia ugonjwa wa Covid-19 tutalazimika tuwaweke wachezaji wote pamoja bila kutangamana na wananchi kuelekea kushiriki mazoezi chini ya makocha wanne wa kigeni wanaotarajiwa kutua nchini baadaye mwezi huu,” meneja huyo alisema na kuongeza kuwa wachezaji hao wana ratiba nzito kwa kuzingatia wataelekea nchini Brazil kwa muda wa mwezi mmoja kushiriki mechi za kupimana nguvu na wenyeji.

Kenya Prisons (Magereza) inayotiwa makali na kocha, Jos Barasa itakosa huduma za wachezaji kama Elizabeth Wanyama, Joan Jelagat, Emmaculate Chemtai, Joy Luseneka, Pamela Masaisai na Lorraine Chebet. Nayo Kenya Pipeline inayojivunia kushiriki kipute hicho mara 19 na kubeba taji mara sita inayofundishwa na kocha, Paul Gitau itazikosa huduma za Gladys Ekaru, Pamela Adhiambo na Agrippina Kundu.

Nayo KCB ya kocha, Japheth Munala inayopigiwa chapuo kushusha ushindani wa kufa mtu kwenye shindano hilo italia na takribani wachezaji nane. Orodha yao inshirikisha: Mercy Moim (nahodha wa Malkia Strikers) Jemimah Siangu, Sharon Chepchumba, Violet Makuto, Leonida Kasaya, Edith Wisa, Immaculate Nekesa na Noel Murambi.

ZILIFUZU

Magereza ilijikatia tiketi ya kushiriki dimba hilo ilipobeba taji la Ligi Kuu ya Voliboli ya Kenya (KVF) msimu uliyotangulia nayo KCB ilimaliza ya pili. Pipeline itashiriki ngarambe hiyo baada ya kuibuka ya tatu kwenye makala ya CAVB yaliyoandaliwa nchini Misri mwaka 2019.

Mabingwa watetezi kwenye ngarambe ya mwaka huu itakuwa Al Ahly ya Misri iliyobeba ubingwa huo kwa mara ya kumi baada ya kucharaza mahasimu wao Carthage ya Tunisia kwa seti 3-1 (21-25, 25-15, 25-11, 25-19 ) katika fainali jijini Cairo, Misri. Nao warembo wa Pipeline walikubali yaishe walipomaliza nafasi ya tatu baada ya kudunga GSP ya Nigeria kwa seti 3-0 (25-22, 25-17, 25-18).

Kwa mara nyingine KCB iliyoibuka ya tisa kwenye makala yaliyopita inapigiwa chapuo kuteremsha kazi nzito kwenye kampeni za mwaka huu.

KCB inalenga kubeba ubingwa huo iliyotwaa mara moja mnamo 2006. Katika historia ya shindano hilo kocha wa KCB, Japheth Munala alipofanya vizuri aliongoza Pipeline kumaliza ya pili mwaka 2015 iliponyukwa seti 3-1 na Al Ahly ya Misri.

Kocha wa Kenya Pipeline anasema kuwa licha ya serikali kusitisha shughuli za michezo nchini timu yake imejipanga kiume kushiriki mashindano hayo. ”Sina shaka kutaja kuwa tumekuwa tushiriki mazoezi makali ninakoamini wachezaji wangu wamekaa vizuri kukabili wapinzani wetu kwenye kinyang’anyiro hicho,” akasema.

Gitau alitwikwa jukumu la kuongoza Pipeline mwaka uliyopita alipotwaa mikoba ya Margaret Indakala ambaye ndiye naibu kocha aliyekuwa akishikilia wadhifa huo baada ya aliyekuwa kocha mkuu, Japheth Munala kujiunga na KCB mwaka 2018.

Licha ya Pipeline kukosa takribani wachezaji sita waliotwaliwa na KCB kwenye kipute cha mwaka 2019, Indakala aliongoza warembo hao kumaliza katika nafasi ya tatu kinyume na yaliokuwa matarajio ya wengi.

Licha ya klabu ya Al Ahly ya Misri kushinda taji hilo mara kumi, kwa jumla klabu za Kenya zinaongoza kuwa kutwaa ubingwa huo mara 13 baada ya kushiriki mara 35. Klabu za Tunisia ambazo zimeshiriki mara kumi zimefanikiwa kushinda ubingwa mara tano huku Algeria ikitawazwa mabingwa mara mbili kutokana mara 11 ambayo klabu zake zimeshiriki.

  • Tags

You can share this post!

Nikipata fursa kuwa Rais sitamhangaisha naibu wangu –...

Asimulia alivyofunza kutumia sanaa kurembesha vifaa