• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:15 PM
Tottenham Hotspur wamfuta kazi kocha Jose Mourinho

Tottenham Hotspur wamfuta kazi kocha Jose Mourinho

Na MASHIRIKA

KOCHA Jose Mourinho amefutwa kazi na Tottenham Hotspur baada ya kudhibiti mikoba ya kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa miezi 17 pekee.

Mkufunzi huyo raia wa Ureno aliaminiwa kuwa mrithi wa Mauricio Pochettino mnamo Novemba 2019 na akaongoza klabu hiyo kukamilisha kampeni za EPL muhula huo katika nafasi ya sita jedwalini.

Kufikia sasa msimu huu, Tottenham wanakamata nafasi ya saba baada ya kujizolea alama mbili pekee kutokana na mechi tatu zilizopita za EPL dhidi ya Newcastle United, Manchester United na Everton.

Isitoshe, Tottenham walidenguliwa na Dinamo Zagreb ya Croatia kwa jumla ya mabao 3-2 kwenye hatua ya 16-bora ya Europa League mnamo Machi 2021.

Tottenham wanamtimua Mourinho siku sita kabla ya kikosi hicho kushuka dimbani kuvaana na Manchester City kwenye fainali ya Carabao Cup itakayowakutanisha uwanjani Wembley, Uingereza mnamo Aprili 25.

Kufikia sasa msimu huu, Mourinho amepoteza jumla ya 10 katika kampeni za EPL, hii ikiwa idadi kubwa zaidi ya michuano kwa mkufunzi huyo wa zamani wa Man-United, Chelsea na Real Madrid kupoteza katika historia yake ya ukufunzi.

Hakuna kikosi kingine ambacho kimepoteza alama nyingi zaidi kutokana na nafasi za kushinda mechi za EPL msimu huu kuliko Tottenham ambao wamedondosha jumla ya pointi 20.

Mnamo Jumapili, Tottenham ilikuwa miongoni mwa klabu sita kuu za EPL zilizotangaza kwamba zitakuwa zikijiunga na kivumbi kipya cha European Super League.

Mechi ya mwisho kwa Mourinho kusimamia kambini mwa Tottenham ni ile iliyowashuhudia waajiri wake wakilazimishiwa sare ya 2-2 dhidi ya Everton mnamo Aprili 16, 2021 uwanjani Goodison Park.

Mourinho amewahi pia kunoa klabu za Benfica (2000), Uniao de Leiria (2001-02), FC Porto (2002-04) na Inter Milan (2008-10).

Joao Sacramento, Nuno Santos, Carlos Lalin na Giovanni Cerra waliokuwa wasaidizi wa Mourinho kambini mwa Tottenham pia wamepigwa kalamu.

“Mourinho na kikosi kizima kilichokuwa kikisaidiana naye katika benchi ya kiufundi ya Tottenham wamekuwa nasi katika kimojawapo vya vipindi vigumu zaidi katika historia ya klabu,” akatanguliza mwenyekiti wa Tottenham, Daniel Levy.

“Ni kocha mtaalamu ambaye ameongoza kikosi kustahimili changamoto tele kipindi hiki cha janga la corona. Katika kiwango cha mtu binafsi, nimejivunia kufanya naye kazi ila yasikitisha kwamba mambo hayajakuwa shwari jinsi sote wawili tulivyotarajia,” akaongeza kinara huyo.

“Anakaribishwa kambini mwa Tottenham wakati wowote na ningependa kumshukuru pamoja na wasaidizi wake wote kwa mchango mkubwa wa kipekee ambao wametoa kwa kikosi tangu Novemba 2019,” akaeleza Levy.

Kiungo wa zamani wa Tottenham, Ryan Mason, ambaye amekuwa akiwatia makali chipukizi wa akademia ya Tottenham sasa atasimamia mechi zilizosalia za waajiri wake muhula huu wa 2020-21.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Murathe asema njama ipo ya kusaidia Raila kutwaa urais wa...

Haaland afunga magoli mawili chini ya dakika nne na...