• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Tusker wazuru Tunis, huku Gor wakisubiri Congo

Tusker wazuru Tunis, huku Gor wakisubiri Congo

Na CECIL ODONGO

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Nchini (KPL) Tusker na Gor Mahia wameimarisha maandalizi kwa mechi zao za kufa kupona wikendi hii katika Kombe la Mashrikisho Afrika (CAF).

Baada ya sare tasa dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia wikendi iliyopita, Tusker itakuwa ugenini ikisaka ushindi au sare ya magoli huku ikilenga kutinga makundi ya Caf. Mechi hiyo itasakatwa Jumapili kuanzia saa mbili usiku katika uga wa Taib Mhiri jijini Sfaxien, Tunisia.

Gor Mahia nao wana mtihani mgumu zaidi wakilenga kubatilisha kichapo cha 1-0 walichopokezwa na AS Otoho d’Oyo ya Jamhuri ya Congo (Brazzaville). Mechi kati ya timu hizo mbili itasakatwa Jumapili ugani Nyayo kuanzia saa tisa mchana.

Kuhusu Tusker, ujumbe wa watu 33 ukiwemo wa wachezaji 26 uliwasili salama salmini jijini Tunis baada ya safari ya saa 12 kutoka nchini ambayo ilipitia Doha, Qatar. Baadaye Tusker, walisafiri kwa basi kutoka Tunis hadi Sfaxien kwa basi safari iliyochukua muda wa saa tatu kabla ya kupumzika katika hoteli yao.

Hivi leo, Tusker wataandaa mazoezi yao ya kwanza asubuhi kisha kesho waandae mazoezi ya mwisho katika uga utakaoandaa mechi hiyo mnamo Jumapili.“Nina imani tutafanya vyema na kutinga hatua ya makundi. Kwa kuwa tutakuwa ugeni, bao lolote tutakalolifunga litakuwa na umuhimu.

Mradi ulinzi wetu na safu yetu ya ushambuliaji iwe wembe na walinzi wetu wawe imara, nina hakika tutatinga hatua ya makundi,” akasema Mkufunzi wa Tusker Robert Matano.Gor nao wanaendeleza mazoezi makali katika Chuo cha KTTC, Gigiri na wamepata afueni baada ya mshambuliaji Jules Ulimwengu na kiungo John Ochieng’ waliokuwa wakizuiliwa jijini Brazzaville kuachiliwa huru baada ya vipimo kuonyesha hawana virusi vya corona tena.

You can share this post!

KK Homeboyz yagonga Tusker

Azma ya Shujaa ni kujiinua Dubai 7s

T L