• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Ubelgiji wakabwa koo na Ugiriki kwenye gozi la kirafiki

Ubelgiji wakabwa koo na Ugiriki kwenye gozi la kirafiki

Na MASHIRIKA

UBELGIJI ambao wanashikilia nambari moja kimataifa kwa mujibu wa viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), walikabwa koo na Ugiriki kwa sare ya 1-1 mnamo Alhamisi usiku.

Ubelgiji wanaotiwa makali na kocha Roberto Martinez walikuwa wakitumia mchuano huo wa kupimana nguvu kujiandaa kwa fainali za Euro ambazo zimeratibiwa kufanyika kati ya Juni 11 na Julai 11.

Ugiriki hawakufuzu kwa kinyang’anyiro hicho kilichoahirishwa kutoka mwaka wa 2020 kwa sababu ya janga la corona.

Ubelgiji waliwekwa kifua mbele na Thorgan Hazard aliyefunga bao lake la sita ndani ya timu ya taifa baada ya kushirikiana vilivyo na Yannick Carrasco katika dakika ya 20.

Kyriakos Papadopoulos alishuhudia mpira alioupiga kwa kichwa ukirejeshwa uwanjani na mhimili wa goli la Ubelgiji kabla ya Georgios Tzavellas kuchuma nafuu kutokana na tukio hilo na kusawazisha mambo.

Ubelgiji walikosa huduma za kiungo matata wa Manchester City, Kevin de Bruyne kwenye mchuano huo. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 29 alipata jeraha la uso, akavunjika pua na kuumia jicho baada ya kugongana na Antonio Rudiger wa Chelsea wakati wa fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) iliyowakutanisha jijini Porto, Ureno mnamo Mei 29, 2021.

Ubelgiji wanaopigiwa upatu kutawazwa mabingwa wa Euro mwaka huu wa 2021 watavaana na Croatia kwenye pambano jingine la kirafiki mnamo Juni 6.

Kikosi hicho kitafungua kampeni za Euro dhidi ya Urusi mnamo Juni 12 kabla ya kuchuana na Denmark mnamo Juni 17. Watakamilisha kampeni zao za Kundi B dhidi ya Finland mnamo Juni 21, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

ICJ, Linda Katiba zashambulia Uhuru

Wilfried Zaha awataka Palace wamwachilie atafute hifadhi...