• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Uganda kukosa kunogesha fainali za AFCON kwa mara ya kwanza tangu 2015

Uganda kukosa kunogesha fainali za AFCON kwa mara ya kwanza tangu 2015

Na MASHIRIKA

MALAWI walicharaza Uganda 1-0 na kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2022 kutoka Kundi B.

Uganda waliingia katika mechi hiyo iliyochezewa jijini Blantyre wakihitaji sare ya aina yoyote ili kufuzu kwa fainali zijazo za AFCON zitakazoandaliwa nchini Cameroon.

Hata hivyo, matumaini yao ya kusonga mbele yalizamishwa na Richard Mbulu aliyefungia Malawi bao la pekee na la ushindi katika dakika ya 15.

Ushindi huo wa Malawi ulitosha kuwakatia tiketi ya kushiriki fainali za AFCON kwa mara ya tatu katika historia. Waliwahi kushiriki fainali za AFCON mnamo 1984 na 2010.

Kichapo ambacho Uganda walipokezwa kilichoendeleza masaibu ya mataifa kutoka Afrika Mashariki ikizingatiwa kwamba Kenya na Tanzania pia walishindwa kufuzu kutoka makundi yao.

Chini ya kocha Meke Mwase, Malawi walifungua kampeni zao za Kundi B kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Sudan Kusini kabla ya kuambulia pakavu dhidi ya Uganda na Burkina Faso ambao kwa sasa wanaongoza Kundi kwa pointi tisa.

Kikosi hicho kililazimishiwa sare na Burkina Faso nyumbani mnamo Novemba 2020 kabla ya kupepeta Sudan Kusini 1-0 ugenini mnamo Jumatano ya wiki iliyopita.

Hadi walipopigwa na Malawi, Uganda hawakuwa wamewahi kukosa kushiriki fainali za AFCON tangu 2015 na walitinga hatua ya 16-bora katika makala ya 2019 yaliyoandaliwa nchini Misri ambapo walidenguliwa na Senegal waliozidiwa ujanja na Algeria kwenye fainali.

Japo Uganda Cranes hawajawahi kutawazwa wafalme wa taji la AFCON, walikuwa wanafainali mnamo 1978.

Chini ya mkufunzi Johnathan McKinstry ambaye ni raia wa Northern Ireland, Uganda walianza vyema kampeni zao za Kundi B kwa kuokota alama saba kutokana na mechi tatu za ufunguzi dhidi ya Burkina Faso, Malawi na Sudan Kusini.

Hata hivyo, kusuasua kwao katika mechi mbili dhidi ya Sudan Kusini na Burkina Faso kuliwavunia pointi moja pekee na kuwaweka katika ulazima wa kukamilisha kampeni za Kundi B katika nafasi ya tatu.

Burkina Faso walikamilisha kampeni za Kundi B kileleni kwa alama 12 baada ya fowadi Bertrand Traore wa Aston Villa kufungia timu yake hiyo ya taifa bao la pekee na la ushindi dhidi ya Sudan Kusini jijini Ouagadougou.

Malawi walikamilisha kampeni zao za makundi kwa alama 10, mbili zaidi kuliko Uganda. Sudan Kusini waliopoteza mechi tano kati ya sita walivuta mkia.

Mechi zote nyinginezo zilizosakatwa mnamo Machi 29 hazikuwa na athari yoyote katika safari ya kufuzu ila baadhi ya matokeo yalichangia nafasi zilizoshikiliwa na timu mbalimbali katika makundi yao.

Mohamed Salah alifunga mabao mawili na kusaidia Misri kupepeta Comoros 4-0 na kukamilisha kampeni zao za Kundi G bila ya kushindwa. Mabao mengine ya Misri ambao ni mabingwa mara saba wa taji la AFCON, yalifumwa wavuni kupitia Mohamed Elneny na Mohamed Sherif.

Comoros walifuzu kwa fainali za AFCON kwa mara ya kwanza baada ya kuambulia nafasi ya pili kundini. Kenya walikamata nafasi ya tatu baada ya kupiga Togo 2-1 jijini Lome.

Mabingwa watetezi wa AFCON, Algeria, waliendeleza rekodi ya kutopigwa hadi mechi 24 baada ya kukamilisha kampeni za Kundi H kileleni. Kikosi hicho kilipepeta Botswana 5-0, mojawapo ya mabao likitokana na penalti iliyojazwa kimiani na kiungo Riyad Mahrez wa Manchester City. Algeria walikamilisha kampeni za makundi kwa mabao 19 kutokana na mechi sita.

Patson Daka alifunga mabao mawili na kusaidia Zambia kupepeta Zimbabwe 2-0 jijini Harare. Zimbabwe waliingia katika mechi hiyo wakiwa tayari wamefuzu huku Zambia waliotawazwa mabingwa wa AFCON mnamo 2012 wakikosa kusonga mbele.

Gabon na Gambia waliofuzu kutoka Kundi D, walipoteza mechi zao za mwisho. Gabon waliokosa huduma za nahodha Pierre-Emerick Aubameyang wa Arsenal, walipigwa 2-0 na Angola jijini Luanda huku Gambia wakipepetwa 1-0 na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGOUganda kukosa kunogesha fainali za AFCON kwa mara ya kwanza tangu 2015

  • Tags

You can share this post!

Martial apata jeraha akichezea Ufaransa dhidi ya Kazakhstan

Afrika Kusini, DR Congo na Angola kati ya vigogo wa soka...