• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 12:52 PM
Uhispania waangusha Italia na kujikatia tiketi ya kuvaana na Croatia kwenye fainali ya Nations League

Uhispania waangusha Italia na kujikatia tiketi ya kuvaana na Croatia kwenye fainali ya Nations League

Na MASHIRIKA

JOSE Luis Mato almaarufu Joselu alifunga bao la dakika za mwisho lililovunia Uhispania ushindi wa 2-1 dhidi ya Italia mnamo Alhamisi usiku na hivyo kufuzu kwa fainali ya Nations League dhidi ya Croatia mnamo Juni 18, 2023.

Yeremy Pino aliwaweka Uhispania kifua mbele katika dakika ya tatu baada ya kumzidi maarifa beki Leonardo Bonucci katika mchuano huo uliosakatiwa mjini Enschede, Uholanzi.

Italia walisawazishiwa na Ciro Immobile aliyepachika wavuni mkwaju wa penalti katika dakika ya 11 baada ya  Robin le Normand aliyekuwa akiwajibikia Uhispania kwa mara ya kwanza, kunawa mpira ndani ya kijisanduku.

Fainali ya Nations League itakayokutanisha Uhispania na Croatia itasakatiwa jijini Rotterdam, Uholanzi.

“Kitu muhimu zaidi kwa sasa ni sisi kushinda hili taji. Hatuwezi kujituma kiasi hicho chote kisha tupoteze dira katika hatua ya mwisho,” akasema kiungo Rodri aliyefungia Manchester City bao la pekee na la ushindi dhidi ya Inter Milan katika fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) nchini Uturuki mnamo Juni 10, 2023.

Taji la mwisho la haiba kubwa kwa Uhispania kujizolea ni la Euro mnamo 2012. Kikosi hicho, almaarufu La Roja, kilizidiwa maarifa na Ufaransa kwenye fainali ya Nations League mnamo 2021. Sasa kitachuana na Croatia wanaowinda taji la kwanza la kimataifa katika historia yao.

Italia watavaana na Uholanzi katika pambano la kutafuta mshindi nambari tatu mapema Jumapili ya Juni 18, 2023 kabla ya fainali. Morocco walidengua Uhispania katika hatua ya 16-bora ya Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar huku Italia wakikosa kabisa kufuzu kwa fainali hizo zilizotamalakiwa na Argentina ambao walifunga Ufaransa penalti 4-2 baada ya sare ya 3-3.

Uhispania na Italia walishuka dimbani kila mmoja akilenga kujinyanyua baada ya kupoteza mechi iliyopita ya kufuzu kwa fainali za Euro 2024. Uingereza walikomoa Italia 2-1 huku Uhispania wakiduwazwa na Scotland kwa kichapo cha 2-0.

Ushindi dhidi ya Italia yalikuwa matokeo ya kuridhisha zaidi kwa kocha mpya wa Uhispania, Luis de la Fuente, aliyejaza nafasi ya Luis Enrique mwishoni mwa fainali za Kombe la Dunia za 2022.

Bao la Joselu dhidi ya Italia liliendeleza ufufuo wa makali ya mvamizi huyo wa Espanyol. Joselu, 33, aliwajibikia Uhispania kwa mara ya kwanza mnamo Machi 2023 na kufikia sasa amepachika wavuni mabao matatu kutokana na mechi tatu za kimataifa.

Aliambulia nafasi ya tatu kwenye orodha ya wafungaji bora wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) msimu huu kwa mabao 16. Japo waajiri wake waliteremshwa ngazi, masogora wa pekee waliomzidi kwa mabao ni Robert Lewandowski wa Barcelona na Karim Benzema ambaye sasa ameyoyomea Saudi Arabia kuchezea Al-Ittihad baada ya kuagana na Real Madrid.

Joselu alifunga mabao manne pekee katika mechi 22 alizochezea Stoke City katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kisha akacheka na nyavu mara sita katika mechi 46 za EPL alizosakatia Newcastle kabla ya kurejea nyumbani kwao Uhispania mnamo 2019.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Msituombe damu ili mkaiuze, wakazi Murang’a wamwambia...

Napoli waajiri kocha Rudi Garcia kujaza pengo la Luciano...

T L