• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Uholanzi katika hatari ya kukosa kunogesha fainali zijazo za Kombe la Dunia

Uholanzi katika hatari ya kukosa kunogesha fainali zijazo za Kombe la Dunia

Na MASHIRIKA

UHOLANZI walifungwa mabao mawili chini ya dakika 10 za mwisho wa kipindi cha pili katika mchuano wa Kundi G kufuzu Kombe la Dunia ulioshuhudia Montenegro wakitoka nyuma na kulazimisha sare ya 2-2 ugani Podgorica City.

Matokeo hayo yaliyumbisha kabisa matumaini ya Uholanzi kujikatia tiketi ya kuelekea Qatar ikizingatiwa kwamba ushindi ungaliwawezesha kufuzu ikisalia mechi moja zaidi. Memphis Depay wa Barcelona alipachika mabao mawili ya Uholanzi katika dakika za 25 na 54 kabla ya Ilija Vukotic na Nikola Vujnovic kusawazisha mambo kunako dakika za 82 na 86 mtawalia.

Licha ya sare, Uholanzi wangali kileleni mwa Kundi D kwa alama 20, mbili zaidi kuliko nambari mbili Uturuki na nambari tatu Norway watakaokutana nao katika mechi ijayo mnamo Novemba 16 jijini Amsterdam.

Sare ya aina yoyote dhidi ya Norway itawezesha Uholanzi kujikatia tiketi ya Kombe la Dunia. Kichapo kitawaweka katika hatari ya kushuka hadi nafasi ya tatu na kukosa tiketi ya kusonga mbele kutegemea matokeo yatakayosajiliwa na Uturuki dhidi ya Montenegro katika mchuano wa mwisho wa Kundi G.

You can share this post!

Ubelgiji wakomoa Estonia na kuingia Kombe la Dunia 2022...

Mbappe afunga mabao manne na kuongoza Ufaransa kufuzu kwa...

T L