• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
Mbappe afunga mabao manne na kuongoza Ufaransa kufuzu kwa Kombe la Dunia 2022

Mbappe afunga mabao manne na kuongoza Ufaransa kufuzu kwa Kombe la Dunia 2022

Na MASHIRIKA

KYLIAN Mbappe alifungia Ufaransa hat-trick (mabao matatu katika mechi moja) yake ya kwanza na kuongoza washikilizi hao wa Kombe la Dunia kusagasaga Kazakhstan 8-0 mnamo Jumamosi katika mchuano wa Kundi D ugani Parc des Princes, Paris.

Ushindi huo uliwezesha Ufaransa wanaotiwa makali na kocha Didier Deschamps kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar. Kikosi hicho kwa sasa kinadhibiti kilele cha Kundi D kwa alama 15, nne zaidi kuliko nambari mbili Finland ikiwa imesalia mechi moja zaidi.

Mbappe aliyepachika kimiani jumla ya magoli manne kati ya manane yaliyofungwa na Ufaransa, alitikisa nyavu za Kazakhstan mara tatu chini ya dakika 30 za ufunguzi wa mechi. Karim Benzema, Adrien Rabiot na Antoine Griezmann aliyefunga penalti ndio wanasoka wengine waliochangia kudhalilishwa kwa Kazakhstan ambao kwa sasa wanavuta mkia wa Kundi D kwa alama tatu kutokana na mechi nane zilizopita.

Hat-trick ya Mbappe ndiyo ya kwanza kwa mchezaji wa Ufaransa katika mchuano wa ushindani mkubwa kimataifa tangu Dominique Rocheteau afanikiwe kufunga idadi hiyo ya mabao dhidi ya Luxembourg mnamo Oktoba 1985.

You can share this post!

Uholanzi katika hatari ya kukosa kunogesha fainali zijazo...

Mke aliyetemwa na mumewe achoma nyumba

T L