• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:55 AM
Uholanzi waanza kutetea taji la Euro 2022 kwa wanawake kwa sare ya 1-1 dhidi ya Uswidi

Uholanzi waanza kutetea taji la Euro 2022 kwa wanawake kwa sare ya 1-1 dhidi ya Uswidi

Na MASHIRIKA

MABINGWA watetezi wa Euro za wanawake, Uholanzi, walifungua kampeni zao za Kundi C kwenye fainali za kipute hicho mwaka huu kwa sare ya 1-1 dhidi ya Uswidi mnamo Jumamosi usiku.

Gozi hilo lilisakatiwa mbele ya mashabiki 21,342 – idadi ya juu zaidi kuwahi kuhudhuria mechi ya Euro za wanawake isiyohusisha nchi mwenyeji katika hatua za makundi.

Uholanzi waliokosa huduma za kipa mzoefu Sari van Veenendaal na beki matata Aniek Nouwen walisawazishiwa na Jill Roord baada ya Uswidi, wanaoshikilia nafasi ya pili kimataifa nyuma ya Amerika, kuwekwa kifua mbele na Jonna Andersson.

Matokeo hayo yaliweka wazi Kundi C ikizingatiwa kuwa Ureno na Uswisi nao walitoshana nguvu kwa sare ya 2-2 katika mchuano wa awali wa kundi hilo ugani Leigh Sports Village.

Uholanzi walinyanyua taji la Euro mnamo 2017 wakinolewa na kocha Sarina Wiegman ambaye sasa anadhibiti mikoba ya Uingereza. Miamba hao kwa sasa wanatiwa makali na Mwingereza Mark Parsons aliyeajiriwa mwaka jana.

Tofauti na Uholanzi wanaomtegemea zaidi fowadi Vivianne Miedema wa Arsenal, Uswidi wanajivunia ufufuo mkubwa wa makali yao tangu waambulie nafasi ya tatu kwenye fainali za Kombe la Dunia 2019 na kuzoa nishani ya fedha kwenye Olimpiki za Tokyo 2020.

Walifuzu kwa fainali za Euro 2022 bila kupoteza mechi 12 mfululizo huku wakiibuka malkia wa Algarve Cup baada ya kuwapiga kumbo Italia, Norway na Ureno mnamo Februari.

Mbali na Ufaransa, Uhispania na Ujerumani ambao ni mabingwa mara nane, Uswidi ndicho kikosi kingine kinachopigiwa upatu wa kutia kapuni taji la Euro mwaka huu. Warembo hao wa mkufunzi Peter Gerhardsson wanawinda taji hilo kwa mara ya kwanza tangu Euro za wanawake zianzishwe mwaka wa 1984.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Euro 2022: Vipusa wa Ureno watoka nyuma na kulazimishia...

Sterling mbioni kuingia Chelsea

T L