• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Ujerumani wakomoa Armenia 6-0 na kutua kileleni mwa Kundi J kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2022

Ujerumani wakomoa Armenia 6-0 na kutua kileleni mwa Kundi J kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2022

Na MASHIRIKA

BAADA ya kuwakomoa Liechtenstein 2-0 mnamo Septemba 2, 2021, Ujerumani waliendeleza ubabe wao dhidi ya Armenia kwa kupokeza kikosi hicho kichapo kinono cha mabao 6-0 mnamo Jumapili katika mchuano wa Kundi J wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

Fowadi Serge Gnabry wa Bayern Munich alifunga mabao mawili chini ya dakika 15 kabla ya Marco Reus na Timo Werner kufunga mengine kufikia mwisho wa kipindi cha kwanza.

Jonas Hofmann alifunga bao la tano la Ujerumani katika dakika ya 52 kabla ya Karim Adeyemi kutokea benchi na kutikisa nyavu za Armenia katika mchuano wake wa kwanza wa kimataifa.

Ushindi huo wa Ujerumani uliwawezesha kuruka Armenia kileleni mwa Kundi J. Chini ya kocha mpya Hansi Flick, Ujerumani kwa sasa wanajivunia alama 12, mbili zaidi kuliko nambari mbili Armenia. Romania wanakamata nafasi ya tatu kwa alama tisa, moja pekee kuliko Macedonia Kaskazini.

Iceland wanashikilia nafasi ya tano kundini kwa pointi nne huku Liechtenstein wakivuta mkia bila alama yoyote.

Chini ya kocha Joachim Loew aliyejiuzulu mnamo Julai na kumpisha Flick aliyetokea Bayern, Ujerumani walibanduliwa na Uingereza katika hatua ya 16-bora kwenye fainali za Euro 2020.

Ujerumani ambao ni wafalme mara nne wa dunia, walinyanyua taji hilo mara ya mwisho mnamo 2014 nchini Brazil.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

WARUI: Serikali iharakishe utoaji chanjo kuokoa sekta ya...

Italia watoka sare na Uswisi na kufikia rekodi ya Brazil ya...