• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 4:54 PM
Ulinzi Starlets kukabana koo na Gusii Starlets katika raundi ya 32 Kombe la FKF

Ulinzi Starlets kukabana koo na Gusii Starlets katika raundi ya 32 Kombe la FKF

NA AREGE RUTH

MABINGWA watetezi wa kombe la Shirikisho la Soka nchini (FKF), Ulinzi Starlets watamenyana na Gusii Starlets ya Ligi ya Taifa ya Divisheni ya kwanza (KWPLD1L) katika raundi ya 32 ya Kombe la FKF.

Katika droo ambayo ilifanywa jana na manahodha wa zamani wa Harambee Starlets Doreen Nabwire na Terry Ouko na kocha wa shule ya upili ya wavulana ya Highway Beldine Odemba, timu 10 za Ligi Kuu ya Wanawake (KWPL), 16 za ligi ya taifa na sita za kaunti zimejumuisha kwenye kinyang’anyiro hicho.

Ulinzi walishinda makala ya kwanza mnamo Oktoba 02, 2021, baada ya kuichapa Vihiga Queens 2-0 kwenye fainali katika Uwanja wa Maonyesho ya Kilimo ya Nakuru (ASK) mjini Nakuru.

Vichuna Vihiga ambao ni vinara wa Ligi KWPL, Gaspo Women na mabingwa watetezi Thika Queens ambao wanashikilia nafasi ya pili na tatu kwenye jedwali, wamejumuishwa kwenye kinyang’anyiro hicho.

Kulingana na Katibu Mkuu wa Vihiga Gilbert Senelewa, huu ni mwaka wa Vihiga kuonyesha ubabe wao baada ya kombe hilo kuwaponyoka mwaka 2021.

“Tutatumia shindano hili kujifunza kutoka kwa timu zingine za ligi. Hii pia ni nafasi ya vilabu vya wanawake kuonyesha talanta zao na pia kukuza talanta za wachezaji mashinani,” alisema Senelwa.

Timu nyingine za KWPL ni pamoja na Nakuru City Queens, Bunyore Starlets, Zetech Sparks, Kisumu All Starlets, Kangemi Ladies na Kayole Starlets.

Naye kocha wa Kayole Collins Tiego amedai kuwa, “Ni mara yetu ya kwanza kushiriki kwenye kombe hili. Katika kila hatua ya pambano hili, tutahakikisha kwamba tumeshinda mechi zetu zote.” 

Mashindano hayo ambayo yalianzishwa rasmi Januari 2020, hayajawahi kufanyika tangu mwaka huo tena baada ya kuhairishwa kutokana na mlipuko wa Covid-19.

Timu za KWPLDV1L zikiwemo Kibera Soccer Ladies, Falling Waters Barcelona, Mombasa Olympics, Sunderland Samba, Soccer Sisters, Eldoret Falcons, Kisped Queens, Bungoma Queens, Gideon Starlets na Royal Starlets pia zimejumuishwa.

Mechi 64 zilichezwa katika raundi ya kwanza  wiki mbili zilizopita, timu zifuatazo zilijikatia tiketi ya raundi ya 32; Moving The Goal Post (MTG), Kahawa Queens, Fortune Ladies, Macmillan Queens, Chuo Kikuu cha Eldoret (UOE), Young Bullets, Kapsabet Starlets, Gusii Starlets, Kolwa Falcons, na Vickers Queens, Coast Starlets na Migori Educational Centre.

Hatua ya 32 itachezwa Machi 18, 2023. Raundi ya 16 inatarajiwa kuanza Aprili 15, 2023. Robo fainali imepangwa kufanyika Mei 20, 2023. Mechi za nusu fainali zitafanyika Juni 24, 2023, na fainali itachezwa Julai 2, 2023.

Kulingana na Nabwire ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Ligi na Mashindano katika FKF anasema, soka ya wanawake itakuwa ya kupigiwa mfano siku zijazo.

“Tumeanza maandalizi ya kufuzu kombe la dunia mwaka 2027. Ninaimani kuwa, ifikapo wakati huo, soka ya wanawake litakuwa la kupigiwa mfano kutokana na mashindano kama haya,” alisema Nabwire.

RATIBA YA MECHI

Vikers Queens vs Royal Starlets

UOE vs Eldoret Falcons

Coast Starlets vs Mombasa Olympic

Kisumu Allstarlets vs MTG United

Kolwa Falcons vs Vihiga Queens

Sunderland Samba vs KISPED Queens

Gusii Starlets vs Ulinzi Starlets

Kangemi Ladies vs Soccer Sisters

Migori Educational Centre vs Thika Queens

Zetech Sparks vs Bungoma Queens

Young Bullets vs Nakuru City Queens

Mac Millan Queens vs Gaspo Women

Kapsabet Starlets vs Kibera Soccer Ladies

Kayole Starlet vs Falling Waters

Kahawa Queens vs Bunyore Starlets

Fortune Ladies vs Gideon Starlets

  • Tags

You can share this post!

Muthama aapishwa kuwa kamishna wa PSC

Mapigano kati ya wanajeshi na M23 yanaendelea kaskazini...

T L