• Nairobi
  • Last Updated February 29th, 2024 6:55 PM
Umiliki wa Newcastle United watwaliwa na mabwanyenye wa Saudi Arabia

Umiliki wa Newcastle United watwaliwa na mabwanyenye wa Saudi Arabia

Na MASHIRIKA

MPANGO wa umiliki wa klabu ya Newcastle United kutwaliwa na Hazina ya Uwezekaji wa Umma (PIF) nchini Saudi Arabia kwa Sh46.8 bilioni umekamilika.

Usimamizi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) umeidhinisha utaratibu huo baada ya kupokea vyeti vya kisheria vinavyohakikisha kwamba Serikali ya Saudi haitadhibiti kwa namna yoyote iwayo uendeshaji wa shughuli mbalimbali za kikosi hicho.

Kwa mujibu wa maagano, PIF itapokeza Newcastle United ufadhili wa asilimia 80 ya fedha za kujiendeshea nyingi za shughuli. Hii ni licha ya Mohammed bin Salman ambaye ni mwana wa kifalme nchini Saudi Arabia kuwa mwenyekiti wa PIF.

Kubadilishwa kwa umiliki wa Newcastle United kunatamatisha ghafla kipindi cha miaka 14 cha kuhudumu kwa Mike Ashley kama mmiliki wa Newcastle United. Ashley ambaye ni Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya Sports Direct, alinunua kikosi cha Newcastle United kwa kima cha Sh20.9 bilioni mnamo Mei 2007.

Idadi kubwa ya mashabiki wa Newcastle United walikongamana nje ya uwanja wa St James’ Park mnamo Oktoba 8, 2021 kusherehekea tukio hilo la kubadilishwa kwa umiliki wa klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Thamani ya mali ya PIF inakadiriwa kufikia pauni 250 bilioni, kiasi cha fedha ambacho sasa kinafanya Newcastle kuwa miongoni mwa klabu tajiri zaidi duniani kwa sasa.

Mara ya mwisho kwa Newcastle United kutwaa taji la haiba kubwa katika ulingo wa soka ni 1955 walipotia kapuni ufalme wa Kombe la FA.

Ashley alitia Newcastle United mnadani kwa mara ya kwanza mnamo Septemba 2008 baada ya mashabiki wa kikosi hicho kuanza kuandamana mara kwa mara baada ya kocha aliyekuwa maarufu zaidi miongoni mwao, Kevin Keegan kujiuzulu. Tangazo la kuuzwa tena kwa klabu hiyo lilitolewa na Ashley mnamo Oktoba 2017.

Kikosi hicho kiliteremshwa ngazi kutoka EPL msimu huo kabla ya kushushwa daraja kwa mara nyingine mnamo 2015-16 japo walijinyanyua upesi na kurejea ligini mwaka mmoja tu kila baada ya kuteremshwa ngazi.

Nafasi bora zaidi ambayo Newcastle United waliwahi kushikilia katika EPL wakiwa chini ya umiliki wa Ashley ni nambari tano mnamo 2011-2012. Chombo chao kilikuwa kikidhibitiwa na kocha Alan Pardew wakati huo.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

KIKOLEZO: Blanda za R. Kelly

Raphinha awabeba Brazil dhidi ya Venezuela katika mechi ya...