• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Ushindi wa kulipa kisasi wa Ulinzi Stars dhidi ya Bandari FC

Ushindi wa kulipa kisasi wa Ulinzi Stars dhidi ya Bandari FC

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

KOCHA wa Bandari FC, Andre Cassa Mbungo amesema kuwa makosa yaliyofanywa na wachezaji wake ndiyo yaliyosababisha kufungwa mabao 3-1 na timu ya Ulinzi Stars FC kwenye pambano la Ligi Kuu ya FKF BetKing iliyofanyika uwanja wa Mbaraki Sports Club jijini Mombasa, Jumanne.

Akizungumza na wanahabari baada ya mwisho wa mchezo huo, Mbungo amesema mastraika wake walipoteza nafasi nyingi za kufunga mabao ambayo yangeliwafanya waibuke washindi kwenye mechi hiyo.

Mbali na upande wa ushambuliaji, Mbungo alidai kuwa hata safu ya ulinzi ilifanya makosa ambayo yalisababisha kuwapatia wapinzani wao mabao hayo matatu.

“Kwa ujumla, makosa tuliyoyafanya ndiyo yaliyofanya tuadhibiwe na Ulinzi Stars ambao tuliwafunga kule kwao,” akasema.

Mkufunzi huyo alisema kuwa kwa ujumla, mechi ilikuwa nzuri isipokuwa matokeo ndiyo yamekuwa mabaya kwao.

“Tunawajibika tujirekebishe makosa haya ili tuweze kufanya vizuri kwenye mechi zetu zijazo,” akasema.

Mbungo anaamini kuwa kusimamishwa kwa mechi kwa kipindi cha mwezi mmoja unusu kumeathiri pakubwa hali ya uchezaji wa wachezaji wake na hivyo, anajaribu awezavyo kurudisha fomu timu ilikuwa kabla ya kusimamishwa kwa michezo kwa sababu ya corona.

“Naamini kama mechi hazikusimamishwa, tungelikuwa mbali kwani fomu yetu ilikuwa iko juu. Lakini tutaendelea kurekebisha makosa timu inayofanya ili turudie hali tuliyokuwa nayo na tupate ushindi mechi zilizobakia za ligi kuu,” akasema Mbungo.

Anaamini kuwa timu itaweza kujirekebisha na ana matumaini makubwa kuwa safu ya ulinzi itaimarika na safu ya ushambuliaji itamakinika na kutumia nafasi itakazopata kufunga mabao ambayo yanaweza kutupatia ushindi kwenye mechi tumebakiza kucheza.

Naye Kocha wa Ulinzi Stars FC Benjamin Nyangweso alisema, ushindi walioupata wa mabao 3-1 dhidi ya Bandari FC ni wa kulipa kisasi cha mabao 2-1 walichofungwa wakati wa mechi ya mkondo wa kwanza ya Ligi Kuu ya FKF Betking iliyochezwa nyumbani kwao.

Nyangweso alisema wachezaji wake walicheza kwa kujituma na kuhakikisha wanapata ushindi ili kulipa kisasi cha kufungwa nyumbani na kuutaja ushindi huo kuwa wa kuwapa morali wanasoka wake kuweza kufanya vizuri kwenye mechi zao zijazo na hasa mchezo wao unaofuata wa Sofapaka.

“Nimefurahi kuwa baada ya kutawala mchezo wa mkondo wa kwanza tuliocheza kwetu na kufungwa, leo tumefika kwao na kuweza kucheza vizuri na kupata ushindi ambao umewapa moyo mkubwa wanasoka wangu kuhakikisha mechi zijazo tinafanya vizuri zaidi,’ akasema kocha huyo wa Ulinzi Stars.

Nyangweso anasema kwa kuwa yeye alikuwa mchezaji, anajua jinsi ya kwenda na wachezaji wake na ndio maana anasikilizana nao.

“Naishi na wachezaji wangu kama ndugu na kukiwa na jambo lolote, tunajadili pamoja na kulitekeleza ama kulirekebisha kwa pamoja,” akasema.

Ulinzi Stars FC iliikomoa Bandari FC kwa mabao 3-1 kwenye mechi ya Ligi Kuu ya FKF BetKing iliyochezwa uwanja wa Mbaraki Sports Club mjini Mombasa juzi Juamnne.

Ulinzi ilistahili ushindi huo kwani ilicheza vizuri zaidi huku kipa wao James Saruni ambaye ni mshika mlango wa Harambee Stars akiwa nyota kwa kuokoa michomo yote yaliyokuwa yakitumwa na mastraika wa Bandari kina Benjamin Mosha, Abdalla Hassan na William Wadri

Ulinzi ilichukua uongozi kunako dakika ya saba kupitia kwa John Kago kabla ya Boniface Onyango kutinga la pili dakika ya 36 kwa mkwaju wa penalti.

Bandari ilipata bao la pekee katika dakika ya 47 mfungaji akiwa William Wadri kupitia penalti.

Lakini aliyekuwa mchezaji wa Bandari miaka ya nyuma, Omar Boraafya aliikatisha tamaa timu yake hiyo ya zamani kwa kuifungia Ulinzi bao la tatu kwenye dakika ya 52.

You can share this post!

Kiungo Eriksen ahakikishia mashabiki kuwa hali yake sasa ni...

Vardy sasa ni mmiliki wa klabu ya soka baada ya kununua...