• Nairobi
  • Last Updated May 14th, 2024 7:52 PM
Vipusa wa Chelsea wacharaza Man-United na kutwaa taji la WSL msimu huu

Vipusa wa Chelsea wacharaza Man-United na kutwaa taji la WSL msimu huu

Na MASHIRIKA

CHELSEA walishinda taji la Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake nchini Uingereza (WSL) kwa mara ya tatu mfululizo baada ya kutandika Manchester United 4-2 katika siku ya mwisho kwenye kampeni za muhula huu mnamo Jumapili.

Sam Kerr alifunga mabao mawili katika kipindi cha pili na kusaidia waajiri wake Chelsea kutoka nyuma na kuzamisha chombo cha wageni wao.

Chelsea walishinda taji kwa alama 56, moja pekee kuliko nambari mbili Arsenal waliopepeta West Ham United 2-0 katika mchuano mwingine wa Jumapili.

Man-United walijivunia uongozi wa 2-1 kufikia mwisho wa kipindi cha kwanza. Ni mara ya kwanza katika historia ya WSL ambapo kikosi kimoja kimejizolea taji hilo mara tatu mfululizo.

Chini ya kocha Emma Hayes, Chelsea kwa sasa huenda wakakamilisha kampeni za msimu huu na mataji mawili ikizingatiwa kwamba watavaana na Manchester City kwenye fainali ya Kombe la FA Cup mnamo Mei 14, 2022 ugani Wembley.

Man-United walikamilisha kampeni za WSL msimu huu katika nafasi ya nne na hivyo watakosa kuwa sehemu ya vikosi vitakavyowania taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao wa 2022-23.

Hayes aliyetawazwa na FIFA kuwa Kocha Bora wa Mwaka mnamo Januari 2022, aliongoza Chelsea kunyanyua taji la kwanza la WSL mnamo 2015. Taji la mwaka huu ni la tano kwa Chelsea kunyanyua chini ya kipindi cha miaka sita.

Washindani wao wakuu, Arsenal, walikamilisha kampeni zao bila taji kwa msimu wa tatu mfululizo. Ushindi wa taji la WSL ni zawadi kubwa kwa wanasoka Ji, Drew Spence na Jonna Andersson watakaoagana rasmi na Chelsea kufikia Juni 2022.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Uhuru ahimizwa akamnadi Raila Mlima Kenya

CHARLES WASONGA: Suala la jisia halifai kutumika na IEBC...

T L