• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 3:57 PM
Uhuru ahimizwa akamnadi Raila Mlima Kenya

Uhuru ahimizwa akamnadi Raila Mlima Kenya

NA KASSIM ADINASI

MBUNGE wa Ugenya, David Ochieng, ambaye pia ni kiongozi wa chama cha MDG, amemrai Rais Uhuru Kenyatta kuanzisha kampeni kali ya kumpigia debe mgombea wa Azimio La Umoja, Raila Odinga, eneo la Kati akisema muda unayoyoma.

Akizungumza Ugenya ambapo alitoa basari kwa watoto maskini, Bw Ochieng alisema Kiongozi wa Taifa hapaswi kusubiri hadi dakika ya mwisho.

“Natumai hivi karibuni tutaanza kumwona Rais akizindua kampeni kali katika eneo la Mlima Kenya kuuza sera ya urais wa Bw Odinga kwa kuwa tumesalia na miezi mitatu pekee kabla ya uchaguzi mkuu. Hakuna muda wa kukaa starehe,” alisema Bw Ochieng.

Kuhusu suala la kumteua Naibu Rais, muunda sheria huyo alisema muungano huo unapaswa kuwa makini.

Bw Ochieng ambaye vilevile ni mshirika katika muungano huo alisema mahojiano yanayofanyika kumtafuta mgombea mwenza wa Bw Odinga yanasababisha kelele ambayo ni hatari kwa muungano huo.

“Njia bora ni kufanya mkutano mbali na vyombo vya habari ambapo wawaniaji waliofuzu watakusanyika na kumteua mtu mmoja kuwa mgombea mwenza. Wanachama wa baraza la Azimio wanaweza kuchukua siku tatu pekee kuamua ni mgombea yupi bora,” alisema Bw Ochieng.

Alieleza kuwa mahojiano hayo yanawapa viongozi wa Kenya Kwanza fursa ya kukashifu muungano wa Azimio mbele ya wapigakura.

“Hili ni jukwaa mwafaka kwa kikosi cha Kenya Kwanza na wanalitumia vyema zaidi, wapigakura wanapowasikiliza wakizungumzia kuhusu jinsi Azimio inavyomdhulumu kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, nyoyo zao zinashushika,” alisema.

Bw Ochieng anayedhamiria kutetea kiti chake cha eneobunge la Ugenya, hata hivyo, amekashifu chama cha ODM kwa kupigia debe mtindo wa ‘suti’ wa upigaji kura katika eneo la Nyanza.

  • Tags

You can share this post!

NJENJE: Pigo kwa wafugaji kuku nchini bei ya mayai ikishuka...

Vipusa wa Chelsea wacharaza Man-United na kutwaa taji la...

T L