• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Vipusa wa Ufaransa wakomoa Italia na kuwapa onyo wapinzani wao kwenye fainali za Euro 2022

Vipusa wa Ufaransa wakomoa Italia na kuwapa onyo wapinzani wao kwenye fainali za Euro 2022

Na MASHIRIKA

WAREMBO wa Ufaransa walituma onyo kali kwa wapinzani wao kwenye fainali za Euro mwaka huu kwa kuponda Italia 5-1 katika mchuano wa ufunguzi wa Kundi D mnamo Jumapili usiku ugani New York, Rotherham, Uingereza.

Grace Geyoro alifungia Ufaransa mabao matatu huku mengine yakifumwa kimiani na Delphine Cascarino na Marie-Antoinette Katoto. Goli la Katoto anayepigiwa upatu wa kunyanyua kiatu cha dhahabu kwenye fainali hizo, lilikuwa lake la 26 kimataifa kutokana na mechi 31 ndani ya jezi za Ufaransa. Italia walifutiwa machozi na Martina Piemonte dakika 14 kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo kupulizwa.

“Tulitaka kudhihirishia mashabiki ukubwa wa uwezo wetu. Wapinzani sasa wana sababu ya kuhofia kukutana nasi. Tulicheza vizuri kuazia dakika ya kwanza,” akasema kocha wa Ufaransa, Corine Diacre.

Ufaransa wanashikilia nafasi ya 14 kimataifa kwa mujibu wa viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na walifuzu kwa fainali za Euro wakijivunia rekodi ya kushinda mechi 14 mfululizo. Hata hivyo, hawajawahi kusonga mbele zaidi ya hatua ya robo-fainali kwenye makala sita yaliyopita ya Euro.

Kwa upande wao, Italia walitazamiwa kutia fora zaidi kwenye fainali za mwaka huu baada ya kudenguliwa mapema katika hatua ya makundi mnamo 2017. Hata hivyo, sasa wanavuta mkia wa Kundi D linalojumuisha pia Ubelgiji waliolazimishiwa sare ya 1-1 na Iceland katika uwanja wa Manchester City Academy. Watavaana na Iceland katika mchuano ujao mnamo Julai 14, 2022 huku Ufaransa wakilenga kuendeleza ubabe wao dhidi ya Ubelgiji.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Akida arefusha mkataba wake na PAOK ya Uturuki

Paul Pogba arejea Juventus baada ya kuondoka Man-United

T L