• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 3:55 PM
Vita vya simba Kenya na Cameroon wakianza dimba la AfroBasket

Vita vya simba Kenya na Cameroon wakianza dimba la AfroBasket

Na GEOFFREY ANENE

Kenya Lionesses inatarajiwa kuwa na kibarua kigumu itakapojibwaga uwanjani kwa mechi yake ya ufunguzi ya Kombe la Afrika la mpira wa vikapu la kinadada dhidi ya Cameroon Lionesses jijini Yaounde, Jumamosi.

Vipusa wa kocha George Mayienga wanatarajiwa kufahamu matokeo yao ya virusi vya corona baadaye Septemba 17 kabla ya kuanza mazoezi ya mashindano hayo ya mataifa 12.

Mabingwa wa Zoni ya Tano ya Afrika, Kenya, walilemewa na Cameroon 61-39 mwaka 2013 nchini Msumbiji na kupoteza 59-55 mwaka 2007 nchini Senegal katika mechi mbili zilizopita kwenye kundi.

Mara ya mwisho Kenya ilipiga Cameroon ilikuwa mwaka 1997 kwa alama 81-68 jijini Nairobi. Mayienga atategemea Mkenya-Mwamerika Victoria Reynolds kuongoza mawindo ya kulipiza kisasi kwenye mchuano huo wa Kundi A.

Mkameruni Ramses Lonlack ndiye mwiba. Kenya itachuana na Cape Verde hapo Septemba 19. Washindi wa kundi hili pamoja na makundi yale mengine matatu wataingia robo-fainali moja kwa moja.

Timu nyingine nchini Cameroon ni Nigeria (mabingwa watetezi), Angola na Msumbiji (Kundi B), Senegal, Misri na Guinea (Kundi C) na Mali, Ivory Coast na Tunisia (Kundi D).

 

  • Tags

You can share this post!

Shujaa yaendea Uhispania kulipiza kisasi raga ya Vancouver...

DOUGLAS MUTUA: Rais Suluhu hasuluhishi, anavuruga