• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
VOLIBOLI: Wafalme Spikers ya Kenya yalipua Misri

VOLIBOLI: Wafalme Spikers ya Kenya yalipua Misri

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya voliboli ya wanaume ya Kenya maarufu kama Wafalme Spikers imejiweka pazuri kufika robo-fainali ya Kombe la Afrika baada ya kupiga Misri kwa mara ya kwanza kabisa.

Vijana wa kocha Gideon Tarus anayesaidiwa na makocha David Lung’aho, Sammy Mulinge na Elisha Aliwa, walishangaza mabingwa hao wa mataji manane ya Afrika kwa seti 3-2 ukumbini Kigali nchini Rwanda.

Kocha Gideon Tarus. Picha/ Maktaba

Wafalme Spikers walianza vibaya mchuano huo kwa kupoteza seti ya kwanza kwa alama 25-19. Hata hivyo, walijikakamua na kuchukua uongozi wa seti 2-1 baada ya kunyakua seti mbili zilizofuata kwa alama 25-22 na 25-20.

Mafirauni walisawazisha seti 2-2 kwa kuzoa ya nne 25-18, lakini Kenya haikuachilia mechi hiyo iwaponyoke ikifanikiwa kuandikisha historia. Ilihitikisha mchezo huo wa kusisimua kwa kutawala seti ya mwisho kwa alama 15-12.

Mchuano huo wa Kundi D ulitangaliwa na Morocco kupepeta Tanzania 3-0 (25-14, 25-14, 25-22). Kenya na Morocco zitavaana hii leo Alhamisi kabla ya Wafalme Spikers kukamilisha mechi za makundi dhidi ya Tanzania hapo Ijumaa.

Katika michuano mingine iliyochezwa Jumatano, Cameroon ililipua Mali 3-0 (25-16, 25-17, 25-22) nayo DR Congo ikaliza Niger 3-2 (28-26, 25-23, 21-25, 21-25, 15-11) katika Kundi C. Tunisia na Nigeria zilianza vyema katika Kundi B. Watunisia walipepeta Waethiopia 3-0 (25-13, 25-14, 25-16) nao Nigeria wakacharaza Sudan Kusini 3-0 (25-20, 25-21, 25-19). Uganda ilizaba Burkina Faso 3-1 (25-15, 25-18, 26-28, 25-13) katika Kundi A.

Tunisia na Cameroon tayari wameshafuzu kushiriki robo-fainali baada ya kuandikisha ushindi mara mbili. Timu mbili za kwanza katika makundi yote manne zinajikatia tiketi ya robo-fainali.

Nafasi nzuri ambayo Kenya imewahi kumaliza dimba hili ni nambari tano mwaka 2007 nchini Afrika Kusini. Timu zitakazofika fainali nchini Rwanda zitaingia mashindano ya dunia yatakayoandaliwa 2022.

You can share this post!

Italia wakomoa Lithuania na kuweka rekodi ya kutopigwa...

Laikipia: Wabunge wawili ndani