• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Waitaliano wanusia kutawala mashanidano ya Migration Gravel Race Maasai Mara

Waitaliano wanusia kutawala mashanidano ya Migration Gravel Race Maasai Mara

Na GEOFFREY ANENE

WAENDESHAJI wa baiskeli Mattia de Marchi na Maria Vittoria Sperotto kutoka Italia wamo mbioni kutwaa ubingwa wa mashindano ya kimataifa ya Migration Gravel Race baada ya mkondo wa tatu kukamilika katika eneo la Maasai Mara, kaunti ya Narok, Jumatatu.

Wawili hao wanaongoza kitengo cha wanaume na kinadada mtawalia baada ya kilomita 429 za kwanza za mbio hizo za kilomita 650.

Marchi, ambaye alikamilisha mkondo wa kwanza (128km) kwa saa nne na dakika 13:33 na mkondo wa pili (172km) kwa saa 6:58:01, anaongoza upande wa wanaume kwa jumla ya saa 15 na dakika saba. Alikamata nafasi ya nne katika mkondo wa tatu (saa tatu na dakika 56). Kwa jumla, Marchi yuko mbele ya Mkenya na mshindi wa mkondo wa kwanza John Kariuki (15:15) na raia wa Australia Lachlan Morton (15:54).

Lachlan alitawala mkondo wa tatu alioshinda kwa muda sawa na Wakenya Suleman Kangangi na Kariuki wa saa tatu na dakika 51. Kwa sababu mfalme wa 2021 Laurens ten Dam kutoka Uholanzi hashiriki mwaka huu, mshindi mpya atatawazwa baada ya mkondo wa mwisho Juni 21.

Suleman, ambaye alitifulia wenzake vumbi katika mkondo wa pili na pia alikamilisha makala yaliyopita katika nafasi ya pili, alikuwa na siku ya kusikitisha Juni 18 baada ya baiskeli yake kuharibika kilomita tano pekee ndani ya mkondo wa kwanza wa kilomita 128 kutoka Taasisi ya Mafunzo ya Mara (MTC) hadi kambi ya Majimoto. Makanika walirekebisha baiskeli na akajikakamua na kukamilisha katika nafasi ya 35.

Mkenya Nancy Akinyi, ambaye alikuwa amepigiwa upatu kuhifadhi taji lake, alipata ajali mbaya katika mkondo wa pili (Majimoto -Morijo Loita), lakini alijikaza akiwa na uchungu na kushinda mkondo huo na uongozi wa jumla. “Hata hivyo, leo (Jumatatu), hakuweza kuanza mashindano kwa sababu ya uchungu kwenye bega lake. Ameaga mashindano,” Mkurugenzi wa mashindano hayo Mikel Delagrange alieleza Taifa Leo.

Raia wa Rwanda Xaverine Nirere pia yuko nje. Alipata ajali Jumapili na kujikaza na kumaliza nambari ya pili. “Alianza mkondo wa tatu, lakini alilazimika kujiondoa katikati ya mkondo huo kutokana na maumivu,” aliongeza Delagrange.

Maria anaongoza kitengo cha kinadada wa jumla ya saa 19 na dakika 25 akifuatwa Lael (saa 19 na dakika 41) na Berber (saa 20 na dakika moja).

Waendeshaji 95 wa baiskeli walianza mashindano Juni 18, lakini baada ya mkondo wa tatu ni 57 wamebaki. Mkenya Geoffrey Langat aliumia vibaya katika mkondo wa pili na kusafirishwa hadi Nairobi kwa matibabu kwa kutumia ndege. “Alijeruhiwa fupa la kiunoni. Aliruhusiwa Jumatatu kuondoka hospitali na atatumia ndege hadi Eldoret anakotoka. Kuhusu Nancy na Xaverine, wametibiwa na madaktari wa mbio hizi na watarejea Nairobi kesho (Juni 21),” aliongeza Delagrange.

Matokeo ya Juni 20:

Wanawake

Maria Vittoria Sperotto (Italia) saa 12 na dakika 47

Berber Kramer (Afrika Kusini) 12:53

Lael Wilcox (Amerika) 13:03

Violette Neza (Rwanda) 13:23

Wanaume

Lachlan Morton (Australia) saa tatu na dakika 51

Suleman Kangangi (Kenya) 3:51

John Kariuki (Kenya) 3:51

Mattia de Marchi (Italia) 3:56

  • Tags

You can share this post!

CUE yamtaka Sakaja ajue haifanyi masihara

Wito waandishi wa habari wamakinike kuelekea uchaguzi mkuu...

T L