• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Wales na Albania waambulia sare tasa kwenye mechi ya kupimana nguvu

Wales na Albania waambulia sare tasa kwenye mechi ya kupimana nguvu

Na MASHIRIKA

TIMU ya taifa ya Wales waliambulia sare tasa dhidi ya Albania katika mchuano wa kirafiki uliowakutanisha Jumamosi kwa minajili ya kujiandaa kwa fainali zijazo za Euro.

Mechi hiyo ilihudhuriwa na mashabiki 6,500 waliokuwa wakirejea uwanjani Cardiff City kwa mara ya kwanza baada ya kipindi cha miezi 18.

Ni gozi lililowapa wanasoka Kieffer Moore na Neco Williams jukwaa la kushirikiana kwenye safu ya mbele ya Wales kwa mara ya kwanza na wakamtatiza pakubwa kipa Gentian Selmani wa Albania.

Licha ya kujivunia idadi kubwa ya wanasoka mahiri na nafuu ya kuchezea mbele ya mashabiki wa nyumbani, Wales walishindwa kuzamisha chombo cha Albania wanaorodheshwa kwa nafasi 49 zaidi chini yao kwa mujibu wa viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Wales watafungua kampeni zao za Euro dhidi ya Uswisi mnamo Juni 12. Mara ya mwisho walipocheza mbele ya mashabiki wao ni katika ushindi wa 2-0 waliosajili dhidi ya Hungary mnamo Novemba 2019. Ushindi huo uliwakatia tiketi ya kunogesha fainali za Euro zilizoahirishwa mwaka wa 2020 kwa sababu ya janga la corona.

Chini ya kocha mshikilizi Robert Page, Wales walitumia mchuano dhidi ya Albania kwa kumwajibisha fowadi Aaron Ramsey wa Juventus kama mshambuliaji mkuu mbele ya nahodha Gareth Bale kwenye mfumo mpya wa 3-4-3 badala ya ule wa 4-2-3-1.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Simba SC yatangaza rasmi kutalikiana na Kahata, kiungo huyo...

Nitapigania ugavana tena katika uchaguzi wa 2022 –...