• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:46 PM
Walibeba taji la Westlands Youth Soccer bila kushindwa

Walibeba taji la Westlands Youth Soccer bila kushindwa

Na PATRICK KILAVUKA

Highridge Girls kutoka kaunti ndogo ya Westlands walishangaza timu zingine kwa kufika kwenye fainali na kuwa shule ya kwanza kubeba taji la Westlands Youth Soccer almaarufu kama Tim Wanyonyi Super Cup, upande wa mabinti kwa mara kwanza bila kudondosha alama.

Mpango wa kujumuisha shule za sekondari katika mpango mzima wa king’ang’anyiro hicho ulikuwa kuinua vipawa vya soka kwa wanafunzi wa kila jinsia eneoni. Timu hii, imekumbatiwa na wachezaji 32.

Chini ya benchi ya kiufundi ya kocha Olga Odiwour, naibu wake Christopher Obiero, timu meneja Kennedy Mutisya, mshirikishi Evans Opicho na kapteni Wendy Anne na ushirikiano wa sako kwa bako kutoka kwa msimamizi wa Shule Grace Otom, timu iliweza kujitahidi kucheza mechi zao na kuibuka mabingwa kwa kuonyesha weledi wa soka na kunyanyua taji.

Katika awamu ya makundi walicharaza St. Martins 2-0, kuwaliza Vetlab 1-0 kabla kuwafyeka Hupendo 6-0. Katika robo fainali, walidengua Shule ya Upili ya North Highridge 6-0 na kufuzu nusu fainali ambapo walikunguta St Martins 2-0 kabla kumaliza udhia wa fainali dhidi ya Vetlab na kuwakomoa 2-0 kupitia wafungaji Brenda Moraa na Juliet Wandata.

Kulingana na Kelvin Otieno Wesonga ambaye alikuwa anasimamia wa michezo hiyo ya mashule, alisema timu hii ilionyesha dalili za kutwaa taji mapema. Baada ya kipute kutamatika, miongoni wa wachezaji wa shule hii walita fora hata na kocha wao Olga Odiwour ambaye pia ni mwalimu wa somo la Kiswahili na Historia na mwanafunzi wa zamani wa Chuo cha Kikuyu alikokuwa akicheza mpira kama winga, walituzwa.

Kocha wa kikosi cha Shule ya Highridge Girls Olga Odiwour akipokea tuzo kwa niaba yake…Picha/PATRICK KILAVUKA

Yeye alitawazwa kocha bora wa kike. Katika usanjari huo, Dan Ondim alikuwa kocha bora kiume. Kipa wao Edna Aluda aliibuka mnyakaji bora huku wa wavulana akiwa Justus Mugambi wa Farasi Lane. Mchezaji Brenda Moraa wa timu alitwaa taji la mfumaji bora kwa kufunga matano kufikia fainali ilhali Daniel Imbezi wa Loresho aliyepachika mabao tisa akituzwa upande wa wavulana.

Mwanasoka wa thamani msichana alikuwa Rebecca Adhiambo ilhali mvulana alikuwa Delvin Wayne Dzeko wa Farasi Lane akarasmishwa. Wachezaji ambao waliibeba timu hii walikuwa nahodha Wendy Anne, mshambulizi Brenda Moraa, mlinda lango Edna Aluda, Straika Juliet Wandata, Winga Lynn Wawire na Melisa Omondi.

Timu hii ilipokea kitita cha Sh 30,000 kikombe, mpira na jezi ikifuatwa na Vetlab Sh20,000 jezi na mpira na Hupendo waliopata Sh10,000 sare na mpira sawia na washindi wa wavulana wa Farasi Lane, Loresho na North Highridge waliopokezwa kiasi sawa mtawalia.

Vigezo vya nidhamu ya juu, mazoezi ya kujituma,kushirikiana kama timu bega kwa bega, ushirikishi mwema kati ya wadau na wachezaji na kiu ya kupata taji vimechochea matokeo ya kuridhisha. Wadau wa timu wanasema mipango uliyoko sasa ni, kufanya mazoezi wakijiandaa kwa mashindano ya shule za upili.

Hata hivyo, wanasema kindumbwedumbwe ambacho wameshiriki kimewapa zoezi tosha la kuendelea kupasha misuli moto. Changamoto ni kwamba, wasicahana wengi hawana buti na fedha za matakwa mingineo ya timu . Wangependa kujisajili katika ligi zenye ushindi za Shirikisho la Soka Kenya majaliwa.

 

Kikosi cha Shule ya Highridge Girls (jezi nyekundu) kikisalimiana na baadhi ya wadau waliosimamia kipute, upande wa shule wakiongozwa na mwalimu mkuu w Shule ya Hospital Hill Bw Bunyasi kabla kucheza fainali dhidi ya Sekondari ya Vetlab…Picha/PATRICK KILAVUKA

You can share this post!

Ndoto la straika huyo ni kuvalia chatu cha Messi

Kibicho afufua mashambulizi dhidi ya Ruto

T L