• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:46 PM
Kibicho afufua mashambulizi dhidi ya Ruto

Kibicho afufua mashambulizi dhidi ya Ruto

Na GEORGE ODIWUOR

KATIBU wa Wizara ya Usalama wa ndani, Dkt Karanja Kibicho , amefufua mashambulizi yake kwa Naibu Rais William Ruto na washirika wake na akahimiza Wakenya kuwachagua viongozi wanaounga handisheki kati ya Rais Uhuru Kenya na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Dkt Kibicho na Dkt Ruto wamekuwa wakishambuliana kuhusu masuala tofauti na siasa za kitaifa.Dkt Ruto na wandani wake wamekuwa wakidai kwamba Dkt Kibicho na maafisa wakuu wa serikali wana njama ya kuhujumu uchaguzi mkuu ujao kwa kumpendelea Bw Odinga.

Hata hivyo, Dkt Kibicho amepuuza wito wa kukoma kushiriki siasa akisema anatekeleza majukumu aliyopatiwa na Rais Kenyatta. Akizungumza Jumamosi katika hafla moja ya kanisa Kaunti ya Homa Bay bila kutaja jina, Dkt Kibicho alishambulia Dkt Ruto akisema nchi haihitaji viongozi wasiokumbatia handisheki kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Dkt Ruto amekuwa akiandaa mikutano ya kampeni kote nchini anayotumia kupuuza marekebisho ya katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) akisema yataongezea Wakenya mzigo mkubwa. Lakini Dkt Kibicho alisema nchi inahitaji marekebisho ya katiba kuwezesha Wakenya kutatua baadhi ya masuala yanayoathiri Wakenya wa kawaida ikiwemo ugavi sawa wa rasilmali.

“Tofauti zetu kama viongozi zinaumiza Wakenya wa kawaida na kuwanyima upatikanaji wa huduma za serikali. Haya yanafanyika wakati kabila moja linathibiti idara ya serikali na raia kutoka kabila lingine wanaamini kwamba hawawezi kusaidiwa kwa sababu hawana mmoja wao hapo,” alisema Dkt Kibicho.

Akizungumza katika kanisa la SDA Odienya, wadi ya Kochia kaunti ndogo ya Rangwe, katibu aliambia Wakenya kuchagua viongozi wanaopigania ushirikishaji wote.Katibu huyo alikuwa ameandamana na mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC), Kasisi Samuel Kobia, kamishna wa tume hiyo, Bw Phillip Okundi na wanachama wengine wa tume hiyo.

Dkt Kibicho alisifu handisheki akisema ilileta mazingira mazuri kwa maafisa wa serikali wakiwemo wale wa polisi eneo la Nyanza.Alieleza kuwa eneo hilo linalojumuisha kaunti za Kisumu, Migori, Homa Bay na Siaya, lilikuwa likikumbwa na ghasia zilizochelewesha maendeleo kabla ya handisheki na kufanya maafisa wa serikali kushindwa kutekeleza miradi ya maendeleo kuwa walichukuliwa kuwa maadui.

“Serikali ilikuwa ikinunua gesi ya kutoa machozi na kutuma nusu yake eneo la Nyanza ambako ilikuwa ikihitajika kwa wingi. Leo, niko na hakika gesi hiyo ya kutoa machozi inaharibika kwa kuwa visa vya ghasia vimepungua,” alitania akiongeza kuwa wakati huu wabunge kutoka eneo hilo hujazana katika ofisi za serikali wakitaka miradi ya maendeleo.

You can share this post!

Walibeba taji la Westlands Youth Soccer bila kushindwa

Inahuzunisha kuona Afrika ikiadhibiwa kwa kutambua Omicron...

T L