• Nairobi
  • Last Updated May 14th, 2024 3:07 PM
Wambui aleta dhahabu ya 2 Olimpiki ya Viziwi 2022

Wambui aleta dhahabu ya 2 Olimpiki ya Viziwi 2022

KENYA iliendelea kufanya vyema katika riadha kwenye Olimpiki ya Viziwi baada ya mtimkaji Ian Wambui kuishindia medali ya pili ya dhahabu katika mbio za mita 1,500 Jumanne.

Linet Nanjala, ambaye Jumatatu alishinda fedha ya mbio za mita 400 kupokezana vijiti akishirikiana na George Waweru, Beryl Wamira na Isaac Atima, kujiongezea shaba ya mita 400.

Wambui alionyesha nia ya kuwazidi wapinzani wake maarifa alipoanza kwa nguvu akifuatiwa kwa karibu na Wakenya wenzake Elikana Rono na Brian Kosgei uwanjani Sesi.

Hata hivyo, Rono na Kosgei walipunguza kasi na kuishia kujuta.

Wambui alijitahidi kuzima ushindani mkali kutoka kwa Mhispania Jaime Martinez na kutwaa taji kwa dakika 3:55.54.

Matinez aliridhika na nafasi ya pili (3:56.18) naye Mjerumani Alexander Bley akafunga tatu-bora (3:57.10).

Rono na Kosgei walikamata nafasi ya nne na nane kwa dakika 3:57.10 na 4:05.58, mtawalia.

“Kwa sababu ilikuwa mara yangu ya kwanza kabisa kushiriki mashindano nje ya Kenya, ushindi huu wa maana sana. Tulianza kwa kasi kwani hatukutaka kubahatisha. Wenzangu walipochoka niliamua kukimbia pekee yangu na kuletea taifa lake ushindi,” alisema Wambui.

Atapata fursa ya kushinda nishani nyingine atakaposhiriki mbio za mita 5,000 ambapo Mkenya Symon Kibai atakuwa akitetea taji.

Kibai alishindia Kenya dhahabu ya kwanza alipotwaa taji la mita 10,000 Jumatatu.

“Ushindi huu ni motisha kubwa kwangu kabla ya kukimbia mita 5,000. Kitakuwa kibarua kigumu kwa sababu Kibai yuko katika orodha ya washiriki, lakini natumai kumpiku,” alisema Wambui.

Bingwa mtetezi wa mita 1,500 John Koech alikuwa shabiki kwa sababu hakufuzu wakati wa mchujo uwanjani Nyayo mwezi Machi.

Hata hivyo, Koech alijikatia tiketi ya kutimka mbio za mita 800. Ameapa kunyakua dhahabu.Nanjala alimaliza nyuma ya raia wa Ukraine, Kristina Kiniankina na Solomiia Kuprych mtawalia.

Kenya sasa ina dhahabu mbili, fedha tatu na shaba nne.

Mwanagofu Isaac Makokha aliingia robo-fainali.

Katika makala yaliyopita mwaka 2017, Makokha alimaliza nambari tano.

Aidha, timu ya soka ya akina dada na mpira wa vikapu ya wanaume zilibanduliwa.

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Wavuvi walioathirika na ujenzi wa Lapsset...

Wanasheria washauri wabunge waondoe makali ya kuumiza raia...

T L