• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
Wanaraga Kabras Sugar tayari kuchezesha densi ‘madeejay’ Homeboyz ligini

Wanaraga Kabras Sugar tayari kuchezesha densi ‘madeejay’ Homeboyz ligini

Na AYUMBA AYODI

MABINGWA watetezi Kabras Sugar wataalika Homeboyz uwanjani Kakamega Showground katika mojawapo ya michuano miwili ya Ligi Kuu ya raga ya wanaume (Kenya Cup) itakayosakatwa Jumamosi.

Mechi ya kudondosha mate kati ya timu ya vyuo vikuu vya Kenyatta (Blak Blad) na Strathmore (Leos) pia ni Januari 28 katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Michuano hiyo ilikuwa imeahirishwa kwa sababu tofauti. Wanasukari wa Kabras pamoja na viongozi KCB ni timu pekee ambazo hazijapoteza mechi kwenye ligi hiyo ya klabu 12.

Nambari tatu Kabras wana alama 29 baada ya kuandikisha ushindi mara sita. Walishinda michuano mitano na alama za bonasi.

Homeboyz waliteremka chini nafasi moja hadi nambari tano wakiwa na pointi 14 baada ya kulimwa na Kenya Harlequin 28-11 wikendi iliyopita. ‘Madeejay’ hao wamezoa ushindi mara tatu na kupoteza idadi sawa ya mechi.

Kabras, ambao walikung’uta Blak Blad 67-3 wikendi iliyopita, watatumai kuchezesha densi Homeboyz baada ya kuwanyamazisha 31-6 mara ya mwisho walikutana msimu 2021-2022.

Blak Blad na Leos wanauguza vichapo vya Jumamosi iliyopita. Leos walichapwa 33-18 na KCB.

Nambari saba Blak Blad wana pointi 13 kutokana na kushinda michuano mitatu na kupoteza mara tatu nao Leos wanapatikana katika nafasi ya tisa kwa pointi 11 baada ya kuzoa ushindi tatu na kupoteza mara tatu.

Kocha wa Kabras, Carlos Katywa amefanya mabadiliko kadhaa katika kikosi kilichozima Blak Blad ikiwemo kujumuisha mzawa wa Fiji, Jone Kubu, kucheza mechi yake ya kwanza. Kubu atajaza nafasi ya Valerian Tendwa.

Wachezaji wa kimataifa wa Uganda, Asuman Mugerwa na Eliphaz Emong watakuwa vizibo vya Joseph Odero na Jeason Misoga naye Brian Juma atajaza nafasi ya Hillary Odhiambo.

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

  • Tags

You can share this post!

Jared Mwanduka: Mwanzilishi wa programu ya LearnsoftERP...

CECIL ODONGO: Jamii ya kimataifa iingilie kati na kufanya...

T L