• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:46 PM
Water yazamisha Cereals Board ligi ya handiboli ya kinadada

Water yazamisha Cereals Board ligi ya handiboli ya kinadada

Na AGNES MAKHANDIA

MABINGWA watetezi Nairobi Water walipepeta mahasimu wao wakuu Cereals Board (NCPB) kwa magoli 31-15 kwenye Ligi Kuu ya Kinadada ya Shirikisho la Handiboli Kenya (KHF) jijini Nairobi hapo Jumamosi.

Water wamekalia juu ya jedwali baada ya ushindi huo dhidi ya mabingwa wa zamani. Wanamaji hao wamezoa alama 10 baada ya kuzoa ushindi mara tano mfululizo. Wameng’oa Nanyuki kileleni. Nanyuki wanashikilia nafasi ya pili kwa alama tisa kutokana na mechi sita.

NCPB inakwamilia katika nafasi ya sita kwa alama mbili baada ya kujibwaga uwanjani mara nne.

Kocha wa NCPB, Dunstan Ashikumu alisalia mwingi wa imani watapata matokeo mazuri licha ya kichapo hicho cha tatu msimu huu.

“Bado tuna muda wa kujinyanyua. Hatujapoteza kila kitu na ninaamini kuwa tutakung’uta timu kadhaa,” mchezaji huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Kenya alisema.

Nahodha wa Nairobi Water, Gladys Chillo alisema kuwa kasi ya juu na uimara wao uliwasaidia kutwaa ushindi.

“Tulianza vyema katika kipindi cha kwanza, lakini tukakosa kufunga magoli wakati fulani kutokana na makosa yetu wenyewe. Hata hivyo, nafurahia kuwa hatujapoteza rekodi yetu ya kuandikisha ushindi,” alisema mchezaji huyo wa timu ya taifa.

Water ilipata mabao yake mengi kupitia kwa Michelle Adhiambo (saba) na Chillo (sita) nao Medina Kerubo na Joan Akinyi wakapachika magoli matatu kila mmoja kwa upande wa Cereals Board.

Katika michuano mingine iliyosakatwa Jumamosi, wanaume wa Chuo Kikuu cha Kenyatta walilemea wenzao kutoka Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta 35-28, huku wale kutoka Chuo Kikuu cha TUK wakitoka nyuma na kubwaga Inspired Boys 25-24.

Ratiba ya Agosti 8 (kuanzia saa tatu asubuhi): Makueni Bees vs KU, Inspired vs Vickers, Buccaneers vs Makueni Bees, Kahawa vs JKUAT, Inspired vs Black Mamba, Tiger vs NCPB. TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

  • Tags

You can share this post!

MAPISHI: Jinsi ya kupika sambusa za nyama

Kenya Lionesses yaimarisha mazoezi kwa mechi ya kufuzu...