• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 8:50 AM
Wazalendo kuvaana na Zamalek mpira wa magongo Afrika

Wazalendo kuvaana na Zamalek mpira wa magongo Afrika

Na AGNES MAKHANDIA

TIMU ya Wazalendo imetiwa katika kundi ngumu la B kwenye mashindano ya Klabu za Afrika za Mpira wa Magongo (ACCC) yatakayoandaliwa ugani Theodosia Ikoh jijini Accra nchini Ghana mnamo Novemba 23-30.

Wawakilishi hao wa pekee wa Kenya wamekutanishwa na washindi wa medali ya fedha mwaka 2018 Halmashauri ya Kukusanya Ushuru nchini Ghana (GRA), washiriki wapya Tairat na miamba Zamalek kutoka Misri katika droo iliyofanywa na Shirikisho la Mpira wa Magongo barani Afrika (AfHF) mnamo Novemba 19.

Mabingwa wa zamani Eastern Company (Misri), wenyeji Ghana Army and Ghana Police pamoja na Kada Stars na Police Machine kutoka Nigeria wako Kundi A.

Katibu Mkuu wa Wazalendo, James Were ameambia Taifa Leo kuwa wamewahi kucheza dhidi ya Zamalek, lakini hawafahamu GRA na Tairat. Wazalendo walipoteza 2-1 dhidi ya Zamalek katika mechi ya kirafiki nchini Misri mwaka 2007.

“GRA ni timu yenye uzoefu kwa sababu imeshiriki mashindano mengi yaliyopita. Hatujui tutarajie nini kutoka kwa klabu za Misri, lakini hatuna presha. Hata hivyo, tuko tayari kwa mashindano na pia kujifunza kutoka kwa klabu nyingine. Tuliomba serikali msaada kwa sababu sisi pekee ni wawakilishi wa Kenya, lakini hatujapata jibu na tunasalia na matumaini,” alisema Were.

Vijana wa kocha Fidhelis Kimanzi wataanza kampeni dhidi ya Zamalek mnamo Novemba 24 (saa kumi na mbili asubuhi) kabla ya kujibwaga uwanjani siku itakayofuata dhidi ya GRA (saa nne unusu asubuhi). Mechi ya mwisho ya Wazalendo ya makundi itakuwa dhidi ya Tairat mnamo Novemba 27 (saa moja asubuhi).

“Kuna joto sana Ghana na tunafurahia kuwa mechi zetu zimepangwa asubuhi. Tutafanyiwa vipimo vya virusi vya corona Jumamosi kabla ya kuelekea Accra,” alisema.

Timu mbili za kwanza katika makundi hayo zitajikatia tiketi kushiriki nusu-fainali.

Wazalendo, ambayo ilipata tiketi ya kushiriki mashindano hayo ilipomaliza Ligi Kuu ya wanaume ya pili nyuma ya Butali Sugar Warriors mwaka 2019, itacheza mechi yake ya mwisho ya kujipima nguvu dhidi ya mabingwa wa zamani Kenya Police hapo Jumamosi saa saba mchana kabla ya kusafiri Jumatatu asubuhi.

Butali pamoja na washindi na nambari mbili wa Ligi Kuu ya kinadada Blazers na USIU mtawalia, hawatakuwa Ghana kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Sharkia kutoka Misri ilibeba mataji ya wanaume na wanawake katika makala yaliyopita nchini Misri mwaka 2019. Haijaingia makala haya.

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

  • Tags

You can share this post!

20 waingia KCB Thika Rally inayofanyika wikendi hii

GWIJI WA WIKI: Quincy Rapando

T L