• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 4:54 PM
GWIJI WA WIKI: Quincy Rapando

GWIJI WA WIKI: Quincy Rapando

Na CHRIS ADUNGO

UIGIZAJI ni sanaa iliyoanza kujikuza ndani ya Quincy Rapando katika umri mdogo.

Japo alisomea uhandisi katika Chuo cha Railway Training Institute (RTI) jijini Nairobi, msukumo wa ndani ya nafsi ulimwelekeza kuzamia masuala ya uanamitindo na muziki wa kufoka.

“Nilianza kusomea uhandisi tayari nikifahamu thamani ya sanaa na nafasi yake katika ujenzi, makuzi na maendeleo ya jamii. Nilitia azma kupalilia vipaji vya uigizaji na uanamuziki ndani yangu japo wazazi hawakuwa wepesi wa kunihimiza kujitosa katika ulingo huo,” asema Rapando.

Rapando alizaliwa na kulelewa jijini Nairobi. Ndiye mwanambee katika familia ya watoto watatu wa Bw George Mulama na Bi Emmy Mulama. Baada ya kusomea katika Shule ya Msingi ya Agbon Academy eneo la Mbotela, alijiunga na Shule ya Upili ya Ruaiveld, Utawala, Nairobi.

Umilisi mkubwa anaojivunia katika Kiswahili na Kiingereza ni upekee unaomweka miongoni mwa walumbi, wafawidhi na waigizaji wanaostahiwa zaidi humu nchini.

Mbali na kufyatulia kampuni na mashirika mbalimbali matangazo ya kibiashara, Rapando pia ni prodyusa wa muziki na mtunzi wa nyimbo za kufoka.

Baadhi ya vibao vyake kufikia sasa ni ‘Dance For Me’, ‘Hype’, ‘Bad Ones’, ‘Execution’ na ‘Narcos’ ambavyo amevicharaza chini ya jina la kisanii, Quincy Ando.

“Sawa na sanaa yoyote nyingine, uigizaji sasa ni kazi ya kitaaluma katika soko pana la ajira ulimwenguni. Mazingira nilimolelewa yalinikuza kilugha na yakanichochea kuvutiwa na michezo ya kuigiza runingani.”

“Niliwakilisha shule yangu katika tamasha mbalimbali za muziki na drama, nikawa maarufu miongoni mwa walimu na wanafunzi wenzangu kutokana na upekee wa kiwango changu cha ubunifu,” anaeleza.

Baada ya milango ya heri kukosa kujifungua katika mchujo wa mchezo ‘Selina’ na filamu ya Netflix ‘40 Sticks’, Rapando alipata fursa ya kuigiza mhusika Thomas katika ‘Maria’ (2019-2020). Huo ndio mchezo uliomkweza katika ngazi ya juu zaidi kwenye ulingo wa uigizaji.

Rapando kwa sasa anaigiza mhusika Kwame katika mchezo ‘Zora’ ambao hufyatuliwa na runinga ya Citizen kila Jumatatu hadi Ijumaa kuanzia saa moja unusu hadi saa mbili usiku.

Sawa na ‘Maria’, ‘Zora’ pia ni mchezo wa kampuni ya Jiffy Pictures inayomilikiwa na wanahabari Lulu Khadija Hassan na Rashid Abdalla.

“Mara nyingine inamjuzu mtu kuchukua hatua ambazo zitachochea maono yake kuwa ndoto zenye thamani maishani. Ingawa ufanisi ninaojivunia katika sanaa ya uigizaji leo hii ni zao la imani, nidhamu, bidii na stahamala; pia ni bahati kubwa ambayo mara nyingine hunishinda kabisa kuelewa,” anakiri Rapando.

You can share this post!

Wazalendo kuvaana na Zamalek mpira wa magongo Afrika

Man-United wasitisha mazungumzo ya kurefusha mkataba wa...

T L