• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
West Ham wakung’uta Leeds United na kupaa hadi nafasi ya tano katika EPL

West Ham wakung’uta Leeds United na kupaa hadi nafasi ya tano katika EPL

Na MASHIRIKA

WEST Ham United walizidi kudhihirisha ari yao ya kutaka kuwa miongoni mwa miongoni mwa vikosi vitakavyoshiriki soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao kwa kuwachabanga Leeds United 2-0 mnamo Jumatatu usiku uwanjani London Stadium.

Ushindi huo uliosajiliwa na masogora wa kocha David Moyes uliwapaisha hadi nafasi ya tano jedwalini kwa alama 48, mbili nyuma ya Chelsea waliosalia katika nambari ya nne baada ya kulaza Everton 2-0 uwanjani Stamford Bridge.

Ingawa hivyo, nafuu zaidi kwa West Ham ni kwamba wana mchuano mmoja zaidi wa kusakata ili kufikia idadi ya mechi ambazo zimepigwa na washindani wao wakuu wakiwemo Chelsea, Leicester City na Manchester United ambao pia wanawania nafasi ya kumaliza kampeni za msimu huu ndani ya orodha ya nne-bora.

Mbali na mabingwa watetezi Liverpool ambao pia wamesakata jumla ya mechi 28 kufikia sasa, klabu nyinginezo zinazowania fursa ya kunogesha kivumbi bara Ulaya msimu ujao ni Everton na Tottenham Hotspur ambao sawa na West Ham, wametandaza mechi 27 kila mmoja.

Jesse Lingard anayechezea West Ham kwa mkopo kutoka Man-United, alicheka na nyavu za Leeds katika dakika ya 21. Bao hilo lilitokana na penalti iliyopigwa na Lingard kabla ya kipa Illan Meslier kumtemea mpira. Mkwaju wa penalti ulitokana na hatua ya beki Luke Ayling wa Leeds kumkabili Lingard visivyo ndani ya kijisanduku.

Bao la pili la West Ham lilijazwa kimiani na Craig Dawson aliyekamilisha krosi ya Aaron Cresswell kwa ustadi mkubwa. Kati ya wanasoka wengine walioridhisha zaidi kambini mwa West Ham ni viungo Declan Rice na Tomas Soucek.

Bao la Lingard lilikuwa lake la sita kufikia sasa kwenye kampeni za EPL tangu ajiunge rasmi na West Ham mnamo Januari. Idadi hiyo ya magoli ndiyo aliyofunga katika jumla ya mechi 38 alizochezea Man-United awali.

Mechi dhidi ya Leeds ilikuwa ya 11 kwa Dawson kuchezeshwa na kocha Moyes tangu amsajili kutoka Watford kwa mkopo mwanzoni mwa mwaka huu. Bao lake lilikuwa la nne akivalia jezi za West Ham katika mashindano yote ya kufikia sasa msimu huu.

Leeds United kwa sasa wanashikilia nafasi ya 11 jedwalini kwa alama 35, tatu nyuma ya Arsenal wanaofunga orodha ya 10-bora chini ya kocha Mikel Arteta.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

SHINA LA UHAI: Ng’amua ukweli kuhusu chanjo ya corona

Mikakati ya kupanua ushiriki wa gozi la UEFA kutoka timu 32...