• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 6:55 AM
Mikakati ya kupanua ushiriki wa gozi la UEFA kutoka timu 32 hadi 36 kuafikiwa mwezi huu

Mikakati ya kupanua ushiriki wa gozi la UEFA kutoka timu 32 hadi 36 kuafikiwa mwezi huu

Na MASHIRIKA

MIPANGO ya kupanua ushiriki wa kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kutoka vikosi 32 hadi 36 kuanzia mwaka wa 2024 inatarajiwa kuafikiwa na wadau kufikia mwisho wa mwezi huu wa Machi 2021.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Klabu za bara Ulaya (ECA), Andrea Agnelli amesema anatarajia mwafaka kuhusu jinsi nafasi nne za ziada zitakavyogawanywa miongoni mwa mataifa wanachama kupatikana chini ya kipindi cha wiki chache zijazo.

Iwapo ECA itafanikisha mchakato huo kwa wakati ufao, basi pendekezo hilo litaidhinishwa na Shirikisho la soka la bara Ulaya (Uefa) mara moja.

Kufaulu kwa mchakato huo kutazima mpango wa kuundwa kwa kampeni mpya ya European Super League (ESL) ambayo imepingwa vikali na Katibu Mkuu wa Uefa, Giorgio Marchetti.

“Umoja wetu utasambaratishwa iwapo baadhi ya mawazo yatakumbatiwa kwa misingi potoshi ya kuvumisha maendeleo ya soka na kufanya mchezo huo kuwa kiwanda kikuu cha ajira na kitega-uchumi kwa wachezaji wa mataifa mbalimbali,” akasema Marchetti.

Ingawa hivyo, maoni yake yalitofautiana pakubwa nay a Agnelli ambaye pia ni mwenyekiti wa kikosi cha Juventus kinachoshiriki Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Mpango wa kupanuliwa kwa ushiriki wa kipute cha UEFA ni wazo asili la aliyekuwa kipa matata wa Manchester United, Edwin van der Sar ambaye kwa sasa ni Afisa Mkuu Mtendaji wa kikosi cha Ajax nchini Uholanzi.

Iwapo mfumo mpya utaidhinishwa, basi badala ya makundi manane ya awali yaliyojumuisha vikosi vinne vya kila kundi vikisakata mechi sita, sasa timu zote zitatandaza mechi 10 dhidi ya nyingine baada ya kupangwa kulingana na uwezo, nguvu na msimamo wao kwenye orodha ya viwango bora vya Uefa.

Matokeo ya mechi hizo zote yataamua msimamo wa jedwali ambapo sasa mechi za mikondo miwili zitapigwa na kila kikosi kuamua washindi watakaofuzu kwa hatua ya mchujo itakayoandaliwa kila baada ya Krismasi.

Hali ikiwa hivyo, basi Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) itakuwa pazuri zaidi kujivunia mshiriki wa tano kwenye UEFA badala ya wanne kwa sasa. Hii ni kwa sababu EPL inachukuliwa kuwa miongoni mwa ligi bora zaidi miongoni mwa kampeni zote za bara Ulaya na vikosi vingi vya kipute hicho vinashikilia nafasi nzuri kwenye orodha ya viwango bora vya Uefa.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

West Ham wakung’uta Leeds United na kupaa hadi nafasi...

‘Kilimo cha miwa Mlima Kenya kina uwezo wa kuvuna...