• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 5:04 PM
Westham tayari kung’ang’ania ligi kuu uingereza

Westham tayari kung’ang’ania ligi kuu uingereza

LONDON, Uingereza

Na MASHIRIKA

KOCHA David Moyes amesema ushindi wa 3-2 uliosajiliwa na West Ham United dhidi ya Liverpool mnamo Jumapili ni ithibati ya ukubwa wa uwezo wa wanasoka wake ambao wana kiu ya kutawazwa wafalme wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) muhula huu.

Kikubwa zaidi kinachomwaminisha Moyes ni kwamba kikosi chake cha West Ham tayari kimefaulu kuzamisha Liverpool, Manchester City, Tottenham Hotspur, Manchester United na Leicester City katika mashindano mbalimbali msimu huu.

Mchuano dhidi ya Liverpool ulikuwa wa nne mfululizo kwa West Ham kushinda ligini na sasa wanashikilia nafasi ya tatu huku pengo la alama tatu pekee likiwatenganisha na Chelsea wanaoselelea kileleni mwa jedwali kwa pointi 26.

Mabingwa watetezi Manchester City wanashikilia nafasi ya pili kwa alama 23 huku Arsenal wakifunga mduara wa tano-bora kwa pointi 20.Chini ya mkufunzi Jurgen Klopp, Liverpool walijitosa ugani London wakipania kuweka rekodi ya kutoshindwa katika michuano 26 mfululizo.

Ushindi dhidi ya West Ham ungaliwaweka mabingwa hao mara 19 wa EPL katika nafasi ya pili na kupunguza pengo la alama kati yao na Chelsea hadi pointi moja pekee.Ilikuwa mara ya kwanza kwa Liverpool kupigwa katika EPL msimu huu baada ya kushinda michuano sita na kuambulia sare mara nne kutokana na mechi 11 zilizopita.

“Sijui kitakachofanyika katika siku, wiki na miezi ijayo. Bado ni mapema sana kubashiri mshindi wa taji la EPL muhula huu. Hata hivyo, maazimio yetu yako wazi – tunalenga ubingwa na mashabiki wetu wana kila sababu ya kuthubutu kuota,” akatanguliza Moyes.

“ Nasi tuna uwezo wa kuweka historia iwapo tutasalia thabiti hadi mwisho wa msimu,” akaongeza.Pablo Fornals na Kurt Zouma walifunga mabao mengine ya West Ham baada ya kipa Alisson Becker wa Liverpool kujifunga.

Trent Alexander-Arnold na Divock Origi walikuwa wafungaji wa magoli ya Liverpool watakaokuwa wenyeji wa Arsenal, FC Porto na Southampton katika mechi tatu zijazo kabla ya kuwaendea Everton, Wolves na AC Milan kwa usanjari huo.

West Ham walikosa pointi mbili pekee ili kukamilisha kampeni za EPL mnamo 2020-21 ndani ya mduara wa nne-bora na hivyo kufuzu kwa kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).Tangu apokezwe mikoba ya West Ham miaka miwili iliyopita, Moyes amefufua makali ya waajiri wake ambao wamejizolea jumla ya alama 65 mwaka huu wa 2021.

Ni Man-City (80) na Chelsea (66) pekee ambao wametia kapuni pointi nyingi zaidi kuliko masogora wa Moyes.Chini ya Moyes ambaye pia amewahi kunoa Everton, Man-United na Real Sociedad, West Ham wamefunga mabao 32 ya EPL kupitia mipira ya ikabu, matano zaidi kuliko kikosi chochote kingine.

You can share this post!

Mshukiwa wa ugaidi taabani

Bandari yalaumu uhuni wa wafuasi Homeboyz

T L