• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 10:55 AM
WYSA United yalenga kileleni michezo ikirejea

WYSA United yalenga kileleni michezo ikirejea

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya WYSA United ni kati ya vikosi vinavyowania tiketi ya kufuzu kupandishwa ngazi kushiriki kampeni za Ligi ya Taifa Daraja la Pili muhula ujao.

Kikosi hiki cha kocha, Turncliff Asiebella ni miongoni mwa timu 14 ambazo zimepangwa Kundi B kuwania taji la Nairobi West Regional League (NWRL) msimu huu.

”Ingawa serikali imesitisha shughuli za michezo kote nchini kwenye juhudi za kuzuia msambao wa virusi vya corona hali ikirejea kawaida tumepania kujituma kiume kuhakikisha tunaendelea kukaa vizuri kuibuka katika nafasi mbili za kwanza,” kocha huyo alisema na kuongeza kwamba raundi hii hawataki mzaha kabisa maana pengine wakiteleza kidogo tu wanaweza kujipata pabaya kama walivyojipata kwenye mechi za kipute hicho msimu uliyopita.

Anaamini msimu huu vijana wake wanatosha mboga kubeba tiketi ya kupandishwa daraja. ”Tuna imani hali ikirejea kawaida na tuendelee kusajili matokeo mema kwenye mechi zetu ili tumalize katika kati ya nafasi nzuri na kusonga mbele. Kwa sasa tumekamata nafasi ya pili katika jedwali hali inayoashiria kuwa tuna uwezo wa kutenda kweli kwenye kampeni za muhula huu.” akasema.

Kwenye msimamo wa kipute hicho, KSG Ogopa FC ingali kifua mbele kwa alama 25 baada ya kupiga mechi tisa. WYSA United ya pili kwa alama 17, moja mbele ya Melta Kabiria sawa na Kemri FC tofauti ikiwa idadi ya mabao. Nacho kikosi cha Red Carpet kinafunga tano bora kwa kukusanya alama 12 sawa na Parklands FC tofauti ikiwa idadi ya mabao baada ya kupiga mechi tisa kila moja.

Nahodha wake, Linus Manoti anasema itawabidi wawe makini zaidi kwa kuzingatia kwa mara nyingine kampeni za muhula hakuna mteremko zinazozidi kushuhudia upinzani wa nguvu. ”Ninashauri wenzangu kuwa mechi zikirejea kamwe walegeze kamba dimbani nia yetu ikiwa kushiriki kila mechi kama fainali,’ alisema na kuongeza watakubali yaishe watakaposhiriki mchezo wa mwisho.

Inajivunia kunoa makucha ya chipukizi wachache na kufanikiwa kujiunga na klabu zingine ambazo hushiriki mechi za ligi tofauti. Orodha yao inashirikisha: Kelvin Etemesi, Denis Atsenga, MacMillan Mugambi (Kangemi Allstars), Rashid Athman Moyo na Simon Madanyi(Dimba Patriots). Pia wapo Kasikasi Victor, Alvin Ajanga Caxton Akaya, Dona Monti na Luice Shihale (Red Carpet).

WYSA United ilizaliwa mwaka 2007 kupitia ushirikiano wao kocha wake mkuu, Turncliff Asiebella, Kelvin Mapesa na Bonface Kagwe lengo kuu likiwa kukuza talanta za wachezaji wanaokuja katika mitaa ya Kangemi na maeneo mengine.

  • Tags

You can share this post!

ERICK GUTO: Nimeshiriki filamu nyingi ila Hullabaloo ndiyo...

Wakazi wa kijiji cha Kihunguro wahangaika baada ya makazi...