• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 6:55 AM
ERICK GUTO: Nimeshiriki filamu nyingi ila Hullabaloo ndiyo naienzi zaidi

ERICK GUTO: Nimeshiriki filamu nyingi ila Hullabaloo ndiyo naienzi zaidi

Na JOHN KIMWERE

ANAORODHESHWA kati ya wasanii wengi tu wa kiume wanaokuja pia wanaopania kuibuka miongoni mwa wanamaigizo maarufu duniani miaka ijayo.

Ni kweli taifa hili limefurika vijana wengi tu wenye vipaji vya uigizaji walivyotunukiwa na Rabuka lakini baadhi yao bado hawajafanikiwa kukubalika wala kutambuliwa.

Erick Ogechi Guto maarufu MC Tall Boy ambaye kando na uigizaji yeye ni mpiga picha pia anamiliki shirika linalokuja kwa jina ‘Hands of Hope Kenya’ ambalo hujihusisha na masuala ya walemavu na wasiojiweza.

Aidha kijana huyu aliyezaliwa mwaka 1996 ndiye aliyeanzisha kundi la uigizaji na runinga ya mtandaoni kwa jina Hollywave Group na Hollywave TV mtawalia.

KEVIN HART

Kupitia kundi hilo anajivunia kuzalisha filamu iitwayo ‘Vituko mitaani’ ilizua gumzo sio haba mwaka jana ambayo huoneshwa kupitia runinga hiyo ya mtandaoni.

”Binafsi nilianza kujituma katika masuala ya uigizaji baada ya kutazama filamu iitwayo ‘Jumaji’ kazi yake mwana maigizo mahiri Kevin Hart mzawa wa Marekani,” chipukizi huyu alisema na kuongeza kuwa wakati huo alikuwa shuleni. Ni miongoni mwa wasanii wanaojivunia kipaji cha uigizaji ingawa bado hawajapata mashiko zaidi kama ilivyo kwa baadhi ya wenzake.

Akizungumza na Taifa leo Dijitali, alisema anataka kutinga upeo wa waigizaji wa kimataifa kama Robert Knepper mzawa wa Marekani anayefahamika kwa uhusika wake kama Theodore ‘T-Bag’ Bagwell kwenye filamu inayokwenda kwa jina Prison Break (2005-2009, 2017).

AMESHIRIKI ZAIDI YA FILAMU 20

Chipukizi huyu anajivunia kufanya kazi na makundi kama Moonbeam Production na Philit Production. Pia anajivunia kushiriki kazi nyingi tu ambazo zimepata mpenyo kupeperushwa kupitia runinga tofauti nchini.

Kati ya mwaka 2018 na 2020 mwana maigizo huyo alishiriki filamu kama ‘Auntie Boss (Maisha Magic East na NTV),’ ‘Inspector Mwala na Papa Shirandula (Zote Citizen TV), ‘Andakava,’ ‘Njoro wa Uba,’ ‘Varshita,’ ‘Selina,’ ‘Hullabaloo Estate,’ na ‘Kina Waters,’ (Zote Maisha Magic East).

”Bila kuongeza kachumbari wala kujipigia debe kwa mara hupenda kutazama filamu ya ‘Hullabaloo’ maana kati ya kazi zangu ndio iliyonivutia zaidi,” akasema.

Kwa wanamaigizo wa kiume hapa nchini anasema angependa sana kufanya kazi na Philip Karanja pia Matayo Keya Makokha. Kwa wasanii wa kigeni angependa kujikuta jukwaa moja nao Samuel Jackson (Marekani) na Leon Schuster maarufu Mr Bones (Afrika Kusini).

Ingawa anapania kukaza buti ili kuibuka kati ya mwigizaji mahiri dunia anasema tangia akiwa mtoto alidhamiria kuhitimu kuwa mzalishaji wa filamu sifika nchini. Anashauri wenzie wawe wavumilivu wala wasivamie tasnia ya uigizaji kwa pupa. Aidha anawahimiza kuwa wabunifu pia kuwekeza kwa miradi tofauti wanapopata mtaji.

Kama kawaida anasema changamoto ni tele maana wapo wasanii wengi tu wanaozidi kuhangaika kwa kukosa ajira. ”Kwa ndani ya kipindi hiki cha janga la corona vibarua vimekuwa haba tena zaidi. Pia ningependa kutoa wito kwa vyombo vya habari hasa mashirika yanayomiliki runinga kuanzisha vipindi nyingi vya kupeperusha filamu za wazalendo ili kutoa ajira kwa wasanii wanaoibukia,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

VALLARY ACHIENG: Ipo siku mtanitazama kwa runinga

WYSA United yalenga kileleni michezo ikirejea