• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Yordenis Ugas wa Cuba amnyuka Many Pacquiao wa Ufilipino na kuhifadhi taji lake la WBA

Yordenis Ugas wa Cuba amnyuka Many Pacquiao wa Ufilipino na kuhifadhi taji lake la WBA

NA CHARLES ONGADI

BONDIA Yordenis Ugas wa Cuba alimnyuka Many Pacquiao wa Ufilipino na kuhifadhi taji lake la WBA kwenye pambano la uzani wa welter katika ukumbi wa T-Mobile Arena, Las Vegas, Marekani, Jumamosi.

Ugas, 35, ambaye ni mshindi wa medali ya fedha katika michezo ya Olimpiki, alivuna ushindi kwa wingi wa alama za 115-113,116-112,116-112 na kuhifadhi taji lake la WBA.

Pacquiao mwenye umri wa miaka 42, alipigiwa upatu kutumia uzoefu wake kumshinda Ugas na kunyanyua taji hili lakini mambo yakawa ndivyo sivyo baada ya kushindwa kukabiliana na wepesi wa mpinzani wake.

Katika pigano hili, Ugas alitumia mbinu ya kujikinga kuepuka ngumi motomoto za mpinzani wake huku akifanya mashambulizi yake kwa ubunifu mkubwa katika raundi za mwanzomwanzo.

Aidha, Pacquiao alishindwa kuhimili ngumi nzito za Ugas kadri mapambano yalivyozidi kuwaka moto katika raundi tano za mwisho.

Ugas alimpokeza Pacquiao ngumi moto moto za kichwa, tumbo na kidevu zilizoishia kumwacha hoi huku akipata jeraha juu la jicho lake la kushoto na nundu chini ya jicho lake la kulia mwisho wa pigano hili la raundi 12.

Pacquiao aliratibiwa kukabiliana na Errel Spence Jr kuwania mataji ya WBC/IBF uzito wa welter ila tu kwa Spence Jr kupata jeraha la jicho siku 11 kabla ya pigano hili na pigano hilo kufutiliwa mbali.

Waandalizi walilazimika kuchukua hatua ya haraka kwa kumleta Yordenis anayemiliki taji la WBA kukabiliana na Pacquiao kuziba nafasi .

Ni mara ya kwanza Ugas kutetea taji hili baada ya kupewa bwerere kutoka kwa Pacquiao aliyeshindwa kulitetea baada ya kipindi cha miezi 28 tangu alipolishinda kwa kumdengua Keith Thuram mwaka wa 2019.

“Nimefurahi kwa kupata ushindi ila nataka kumpongeza Pacquiao kwa kunipa fursa hii kupambana naye, namheshimu lakini niliwaambia awali kwamba mimi ndiye bingwa wa WBA “ akajigamba Ugas baada ya pigano hili.

Lakini Pacquiao alidai hakujiandaa barabara kwa pigano hili baada ya mabadiliko ya ghafla baada ya jeraha la Spence Jr.

Pacquiao anayekumbukwa kwa pigano lake la mwaka wa 2015 dhidi ya Flyod Maywether sasa ana rekodi ya kushinda mapigano 62, 39 akishinda kwa njia ya KO na kushindwa mara 8 na kuandikisha matokeo ya sare mara 2.

Kwa upande wake, Ugas ameshinda mapigano 27 , akishinda mapigano 12 kwa njia ya KO na kushindwa mara 4.

Wakati huo viongozi wa ndondi Pwani wamempongeza bondia Rayton ‘Boom Boom’ Okwiri kutokana na ushindi dhidi ya Fidel Munoz wa Colombia nchini Marekani wiki iliyopita.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Ndondi Mombasa Abdulsalaam Kassim na naibu wake John Andakasia wamepongeza Okwiri kwa ushindi na kuwaomba mabondia wa Mombasa na Pwani kufuata nyayo za bingwa huyu aliyeanza mchezo wake katika klabu ya Tudor, Mombasa.

You can share this post!

Serikali kutafutia bandari biashara

Askofu akubali atamlea na kumtunza mtoto aliyezaa na...