• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Amri ya kusitisha mikutano yapoza joto la kisiasa

Amri ya kusitisha mikutano yapoza joto la kisiasa

Na WAANDISHI WETU

IDADI kubwa ya viongozi wa kisiasa wikendi walitii amri ya Rais Uhuru Kenyatta kusitisha mikutano ya hadhara.Tofauti na wikendi zilizopita, wanasiasa wengi hawakuonekana hadharani tangu Jumamosi na baadhi yao walitokea jana walipoenda makanisani.

Wawaniaji wa useneta katika Kaunti ya Machakos jana walitumia makanisa kujipigia debe ambapo walihimiza waumini kuwachagua katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Alhamisi, wiki hii.

Baada ya kuondoka kanisani, wanasiasa hao walielekea nyumbani kwao tofauti na awali ambapo walimaliza ibada na kukutana na wananchi kando ya barabara.

“Tulikuwa tumepanga mkutano mkubwa katika eneo la Mavoko. Lakini kwa sababu serikali imepiga marufuku mikutano ya kisiasa katika juhudi za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona nchini, tumeamua kuzunguka makanisani,” akasema kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka baada ya ibada katika kanisa la AIC Muumandu.

Baadaye, makamu huyo wa rais wa zamani aliyekuwa ameandamana na mwaniaji wa useneta wa Wiper Agnes Kavindu Muthama, alikutana na vikosi vya kampeni vya chama hicho vilivyokuwa vimetumwa katika makanisa mbalimbali kumpigia debe mgombeaji wao.Waliwataka wakazi wa kaunti hiyo kujitokeza kwa wingi kuchagua Bi Kavindu mnamo Machi 18.

Bi Kavindu anakabiliwa na ushindani kutoka kwa Mutua Katuku (Maendeleo Chap Chap), Urbanus Muthama Ngengele (UDA), John Musingi (Muungano), Stanley Masai Muindi (Economic Democracy), Edward Musembi Otto (Ford Asili) na Simeon Kioko Kitheka (Grand Dream Development) kati ya wengineo.

Katika Kaunti ya Kilifi, mbunge wa Malindi Aisha Jumwa na mwenzake wa Kilifi Kaskazini Owen Baya ambao wamekuwa mstari wa mbele kufanya mikutano ya kumpigia debe Naibu wa Rais William Ruto, wikendi hawakuonekana hadharani.Bi Jumwa ambaye ametangaza nia ya kuwania kiti cha ugavana wa Kilifi katika uchaguzi mkuu wa 2022, alikuwa ameanza kampeni za mapema.

Rais Uhuru Kenyatta Ijumaa alipiga marufuku mikutano kwa siku 30 katika juhudi za kupunguza maambukizi ya virusi vya corona nchini. Rais Kenyatta aliagiza polisi pamoja na makamishna wa kaunti na wilaya kukamata wanasiasa watakaopatikana wakifanya mikutano ya kisiasa.

Mwisho wa kuonekana hadharani kwa Bw Baya ilikuwa ni Ijumaa kabla ya Rais Kenyatta kutangaza marufuku hiyo, ambapo alihudhuria hafla ya Kamati ya Usalama ya Bunge kutetea haki za Wapemba kupata uraia wa Kenya na kuzinduliwa kwa kituo cha umeme eneo la Tezo.

Nao Bi Jumwa na Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi pia hawajaonekana hadharani wakifanya mikutano tangu Jumatatu walipoongoza sherehe ya kusherehekea siku ya wanawake ulimwenguni eneo la Vipingo.Hata hivyo, mnamo Jumamosi, wanasiasa wakuu kutoka eneo la Magharibi walipuuzilia mbali agizo la Rais Kenyatta na kuhudhuria mazishi kijijini Matili, eneobunge la Kimilili, Kaunti ya Bungoma.

Viongozi hao wakiongozwa na kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang’ula na spika wa Seneti Kenneth Lusaka walihudhuria mazishi ya mjomba wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Shirika la Biashara la Kimataifa (UNCTAD) Mukhisa Kituyi.

Kwa mujibu wa agizo la Rais Kenyatta, mazishi yanafaa kuhudhuriwa na jamaa wa karibu wa mwendazake na idadi ya waombolezaji isiyozidi watu 100.

Ripoti za Pius Maundu, Charles Lwanga, Brian Ojamaa na Onyango K’onyango

You can share this post!

Hofu uvamizi wa nzige unapunguza asali

CHARLES WASONGA: Rais Kenyatta, Mama wa Taifa na Kagwe sasa...