• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 6:21 PM
Angika daluga za ulingo wa kisiasa, Kidero amwambia Raila

Angika daluga za ulingo wa kisiasa, Kidero amwambia Raila

NA GEORGE ODIWUOR

ALIYEKUWA Gavana wa Nairobi Evans Kidero, amemtaka kiongozi wa Azimio Raila Odinga kustaafu kutoka siasa na kutwika mtu mwingine wajibu wa kuwa msemaji wa jamii ya Waluo.

Dkt Kidero alipendekeza kuwa mtu mwingine anapaswa kuwa kiongozi wa kisiasa wa jamii hiyo.

Bw Odinga, kupitia chama chake cha ODM amedhibiti siasa katika kaunti za Kisumu, Siaya, Migori na Homa Bay kwa miaka mingi.

Kulingana na Dkt Kidero, waziri mkuu huyo wa zamani amekuwa katika siasa kwa miaka mingi na anafaa kupumzika na kupisha mtu mwingine kuongoza siasa za eneo hilo.

Dkt Kidero alisema mtu huyo anaweza kuchaguliwa na kiongozi huyo wa ODM mwenyewe.

“Raila anapaswa kuondoka katika wadhifa wake na kupisha mtu mwingine anayejua anatosha kwa kiti hicho. Ni kawaida ya kila shirika kuwa na warithi wa kila wadhifa wa uongozi,” alisema.

Hata hivyo, Dkt Kidero alikataa kutaja anayepaswa kumrithi kiongozi huyo wa Azimio.

Bw Odinga amewahi kuhimizwsa kustaafu siasa huku baadhi ya wakosoaji wake, akiwemo Rais William Ruto wakimwambia ameshiriki siasa kwa muda mrefu.

Hii ni baada ya waziri mkuu huyo wa zamani kugombea urais mara tano na kushindwa na wapinzani tofauti.

Dkt Kidero amekuwa akitajwa kama mmoja wa watu wanaopaswa kumrithi kama msemaji wa jamii ya Waluo.

Wakati wa kampeni za uchaguzi wa ugavana kaunti ya Homa Bay, Gavana Gladys Wanga alimlaumu Dkt Kidero kwa kugombea kiti hicho ili kumbandua Bw Odinga kama kigogo wa siasa wa jamii ya Waluo.

Hata hivyo, wakati huo, Dkt Kidero alisema hakumezea mate wadhifa huo.

“Sitaki kuwa msemaji wa Waluo. Lengo langu ni kuunganisha jamii,” alisema.

  • Tags

You can share this post!

DOUGLAS MUTUA: Jumatatu si sikukuu rasmi

WANDERI KAMAU: Kwa kuwatoza ‘mama-mboga na boda’ ada...

T L